Imeandikwa na Ikunda Erick
WABUNGE wanane wa Chama cha Wananchi (CUF) waliovuliwa uanachama na
chama hicho wamepinga hatua hiyo na kutishia kwenda mahakamani kutafuta
haki yao.
Wakati wabunge hao wakisema hayo, Wakili wa siku nyingi, Tamila
Makene alisema uamuzi wa chama cha siasa kuwavua uanachama wabunge ni
uamuzi sahihi kwa mujibu wa Katiba ya nchi Ibara ya 71 kifungo kidogo
1(f). Tamila alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumzia jambo
hilo kisheria na kusema chama cha siasa ndicho kina mtambua mwanachama
wake na kwamba chama hicho hicho ndicho kinachoweza kumvua uachama pia.
“Kama chama kimetoa taarifa kuthibitisha kuwavua uanachama wabunge
hao ni sahihi kwa sababu hata Katiba inatambua na inaelezea ukomo wa
mbunge kwenye Ibara ya 71 kifungu kidogo cha kwanza (f), sasa kama
wataamua kwenda mahakamani ni jambo jingine,” alisema Makene.
Wakizungumzia kuvuliwa kwao uanachama, Kiongozi wa Wabunge wa CUF,
bungeni ambaye naye amevuliwa uanachama, Riziki Ngwali alisema hadi sasa
hawajapokea barua rasmi ya kuvuliwa uanachama wao na kusisitiza kwamba
walichaguliwa kwa barua na lazima watenguliwe kwa barua.
“Hatujapokea barua hadi sasa, lakini pamoja na hilo, sisi hatukubali
uamuzi huo kwa sababu haujatolewa na mamlaka sahihi, tumeamua kwenda
mahakamani kutafuta haki yetu,” alisema Ngwali. Kaimu Naibu Katibu Mkuu
wa CUF-Bara, Jafar Mneke alisema kati ya wabunge 10 wa viti maalumu wa
chama hicho, wawili ndio wamesamehewa baada ya kutoa ushirikiano na
Baraza la Maadili la chama hicho, lilipowahitaji wabunge wote hao
kuwahoji.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment