Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amekabidhi
hatimiliki 88 kwa wakazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam kati ya 4333
ambazo ziko kwenye hatua za mwisho katika mradi wa urasimishaji wa
makazi holela.
Akikabidhi hatimiliki hizo, Mhe. Lukuvi amesema
hizi hati ni mtaji uliofufuliwa baada ya wakazi kukakaa na kuendeleza
maeneo yasiyopimwa yaani mtaji mfu kwani hakuna mtu yeyote ambaye
angewezakupata mkopo bila hati.
Mhe. Lukuvi amesema kuwa Serikali
ya Aawamu ya Tano inayo dhamira ya dhati ya kurasimisha makazi nchi
nzima ili kuongeza thamani ya ardhi au maeneo husika. Ardhi yenye
hatimiliki thamani yake inaongezeka kwani inatambuliwa na taasisi za
fedha ambazo ni rahisi kukuopesha wenye hati.
“Kwa hati hizi
zilizotolewa takribani 4333 tukisema kila nyumba ikopeshwe kwa kiwango
cha chini cha shilingi milioni 10, kwa siku ya leo Kimara inapata mtaji
wa karibu bilioni 40.5,”alisema Mhe. Lukuvi.
Aliongeza kuwa
maeneo yote ya miji ambayo hayajapimwa, yapimwe na halmashauri na
manispaa zote nchini ili kuyaongezea thamani na kuondokana adha ya watu
kujenga kwenye makazi holela.
Waziri huyo wa Ardhi amesema kuwa
kwa sasa wakazi wa Kimara wameondoka kwenye kuitwa watu wanaokaa kwenye
makazi holela na sasa wanajulikana kuwa wakazi wa maeneo rasmi.
Aidha,
Mhe. Lukuvi ametoa onyo kali kwa matepeli wa ardhi kuacha vitendo hivyo
mara moja kwani dawa yao ipo tayari. Ameongeza kuwa na madalali uchwara
wa ardhi waache tabia ya kuwaonea wanyonge na kusababisha mali zao
ziuzwe kwa njia ya udanganyifu.
“Hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya matapeli hao ambao wamekuwa wakishirikiana na
baadhi ya maafisa wasiowaaminifu,”alisisitiza Lukuvi.
Amewaonya
wanaotunza mapori mijini kuwa wakae makini kwani watanyang’anywa
wasipoendeleza maeneo hayo. Ameongeza kuwa na wale waliokuwa wanamiliki
maeneo makubwa bila kuwa na hati itabidi waanze kulipa kodi ya pango la
ardhi ili Serikali ipate mapato.
Kwa upande wake, Meya wa
Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amempongeza Mhe. Lukuvi kuwa ni mtu
anayejali maendeleo ya wananchi bila kujali vyama vyao wala itikadi zao.
Amesema Lukuvi anafuata nyayo za Mhe. Rais John Pombe Magufuli ambaye
anafanya maendeleo kwa watanzania wote bila kujali vyama vyao.
Hivyo,
amewataka wanasiasa wengine waige mfano wa Mhe. Rais Magufuli na
William Lukuvi ili kuwaletea wananchi maendeleo pasipokuangalia vyama
wala dini.
Naye mkazi wa Kilungule, Kimara ambaye amekadhiwa hati
na Mhe. Lukuvi, Bwana Prackson Lugazia amesema hatua hii ya kupata hati
ni jambo zuri na la kimaendeleo kwani ataweza kupata mikopo kwenye
taasisi za fedha kwa kutumia hati hiyo.
“Nimefurahi sana kupata hati hii kwani kwa sasa ardhi yangu imeongezeka thamani kuliko ilivyokuwa awali,” alisema Lugazia.
Hati
hizo zimetolewa kwenye mpango wa Urasmishaji wa Makazi Holela katika
kata za Saranga na Kimara, jijini Dar es Salaam. Mpango huu umesimamiwa
na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na ni mpango darasa
ambao unaweka msingi kwa ajili ya urasimishaji wa makazi nchi nzima.
0 comments:
Post a Comment