Imeandikwa na Lucy Lyatuu
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
ameendelea kusikiliza mashauri ya migogoro ya ardhi jijini Dar es Salaam
na kubaini kuwepo kwa mafisadi wa utapeli wa ardhi wanaoshirikiana na
maofisa ardhi.
Pamoja na hayo, waziri huyo amebainisha kuwa wakazi wengi wa jiji
hilo wamekuwa wakimiliki ardhi kutokana na hati feki na tayari amefuta
hati 180 zilizokuwa zimedhulumiwa na maeneo hayo kurudishwa kwa
wenyewe.Lukuvi alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akisikiliza
mashauri mbalimbali yanayohusu migogoro ya ardhi ndani ya jiji hilo kwa
lengo la kuyatatua.
Alisema kuanzia juzi amesikiliza mashauri 99 na sehemu kubwa ya
matatizo hayo yamesababishwa na watendaji wa serikali wakiwemo pia
maofisa ardhi ambao wameanza kudhulumu wananchi ardhi tangu kipindi cha
uongozi wa awamu ya kwanza hadi sasa. Alibainisha kuwa matapeli hao wa
ardhi, walifikia hatua ya kuthubutu hadi kuchovya hati katika majani ya
chai ili kuonekana ni ya zamani.
Alitoa mfano wa moja ya shauri alilosikiliza na kumbaini mkazi wa
jijini hilo mwenye asili ya Kiarabu aliyetambuliwa kwa jina la Omar
Mohamed Agil, anayetumia Kampuni ya Holland Investment, anayedaiwa
kuchukua viwanja vya watu na kughushi hati na hata kuweza kuitumia kwa
kukopa benki kiasi cha Sh milioni 300. “Omar aliweza kuingia ubia na
mzee mmoja mkazi wa Mtoni na kisha kuchukua hati ya mzee huyo na kwenda
kukopea benki.
Alienda hadi mkoani Mtwara na kutumia hati hiyo hiyo kwa kushirikiana
na mjomba wake anayejulikana kwa jina la Hassan Salum ambaye naye
amemjumuisha kuwa mbia wa hati hiyo na kwenda Benki ya Amana na kukopa
shilingi milioni mia tatu,” alisema Lukuvi.
Aidha, alisema mtuhumiwa huyo pia alikwenda eneo la Kawe Mzimuni kwa
mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Hamida Simba, na kuchukua hati
ya mwanamke huyo na kuitoa nakala kivuli ya hati hiyo na kurudisha feki
na kuondoka na halali. Kutokana na hayo aliyoyabaini, aliagiza kuwa ni
marufuku kwa watendaji wote katika ofisi za ardhi nchini kufanya miamala
yoyote ya hati, nyaraka ama kupokea chochote kutoka kwa mtuhumiwa huyo.
“Lakini pia nawaonya matapeli kutojaribu tena kunyang’anya raia ardhi
zao, kwani sasa wamejulikana na hata hata wale wenye tabia ya kutumwa
wizarani ni marufuku kuingia katika jengo hilo,” aliagiza Lukuvi.
Akizungumzia hali ya utapeli wa viwanja katika jiji hilo, alisema hali
ni mbaya kwani wananchi wengi wamedhulumiwa viwanja vyao wakapewa watu
wengine, wengine wamejenga kwenye ardhi wasizomiliki, wametapeliwa na
wengine wamepewa hati feki.
Alisema yapo maeneo ambayo hupimwa zaidi ya mara moja na watendaji
hali inayosababisha watu wengi kumiliki eneo moja ambalo halitoshi,
lakini watendaji hao hawajali bali huyapatia maeneo hayo michoro yote
kuanzia wizarani hadi wilaya.
Lukuvi alisema pia kuna matapeli wanaokwenda kutembelea maeneo yaliyo
wazi halafu wanakwenda ofisi za Halmashauri na maofisa ardhi na kuwapa
ofa stahiki za watu wanaomiliki na wanapogundua anayemiliki ni nani wao
hutengeneza ofa nyingine, halafu ofisa ardhi anasaini na kuchomoa ile
ambayo ni halali katika faili na kuchomeka feki.
“Ili mpango huo uweze kufanikiwa, maofisa hao hubadili hata mwaka wa
ofa hiyo na kuweka wa mwanzo zaidi, na ili ionekane kwamba ni ya zamani,
hata hiyo huichovya katika majani ya chai na kuirudisha katika file,”
alisema na kuongeza kuwa katika hati hufanya hivyo hivyo kwa kuchapa
upya na kuweka mhuri na kuiga saini.
Alisema kwa wale wote waliokutwa na madhara hayo ya kuvamiwa na
kunyang’anywa, serikali inarudisha ardhi kwa anayestahili na
waliodhulumiwa na maofisa wa serikali, wanapewa maene mengine mbadala.
“Mpaka sasa watu 700 wameshapewa viwanja katika eneo la Pemba mnazi,
Kigamboni, ili kuwafuta machozi kutokana na kudhululiwa huku,”
alifafanua Lukuvi. Alisema watendaji waliofanya utapeli huo pamoja na
kwamba wapo baadhi walishastaafu, waliopo kazini watachukuliwa hatua na
tayari waliobainika wameshaanza kufukuzwa na kusimamishwa kazi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment