Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » RIADHA WAAHIDI MEDALI LONDON WAKIAGWA DAR

RIADHA WAAHIDI MEDALI LONDON WAKIAGWA DAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


MWANARIADHA aliyeipeperusha vema Bendera ya Tanzania katika mashindano ya Mumbai Marathon, Alphonce Simbu, amesema watahakikisha timu ya Taifa ya Riadha Tanzania, inarejea na medali katika michuano ya Dunia itakayoanza kutimua vumbi kesho jijini London, Uingereza.


Akizungumza jijini Dar es Salaam mara tu baada ya timu hiyo kukabidhiwa Bendera ya Taifa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, Simbu ambaye atashiriki mbio ndefu za kilomita 42 (full marathon), alisema wamejiandaa kikamilifu na wanajua wanabeba dhamana kubwa kwa Watanzania wote, hivyo watahakikisha wanapambana na kuleta medali nyumbani.

Alisema wamejiandaa vizuri na makocha wamefanya kazi kubwa, hivyo kilichobaki ni kwa Watanzania wote kuwaombea na pia kuhakikisha wanawashuhudia moja kwa moja kupitia DStv kuona jinsi watakavyoiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo.

Jumla ya wanariadha watano watashiriki mbio za kilomita 42 ambao ni Simbu mwenye rekodi ya 2:09.10- aliyoiweka hivi karibuni katika mashindano ya London Marathon 2017, Ezekiel Jafari ( 2:11.55 -Hannover Marathon 2017), Stephano Gwandu (2:14.18- Tunis Marathon), Sara Ramadhani (2:33.08- Dusseldorf Marathon 2017) na Magdalena Shauri (2:33.28-Hamburg Marathon 2017).

Wanariadha wengine watatu waliopo katika timu hiyo inayoondoka leo kuelekea London watashiriki mbio fupi ambapo Gabriel Gerald na Emanuel Giniki watashiriki mita 5,000 wakati Failuna Abdi yeye akishiriki mita 10,000.

Kwa upande wa Waziri Mwakyembe mbali ya kuipongeza Multichoice Tanzania (DStv) kwa jitihada kubwa walizozifanya katika kuhakikisha timu hiyo inafanikiwa kufanya mazoezi na maandalizi, alisema ameridhishwa na namna timu hiyo ilivyojiandaa na kwamba wizara yake iko bega kwa bega na wadau wa michezo hapa nchini katika kuhakikisha tunapiga hatua katika sekta ya michezo.

“Kwanza kabisa nimetiwa moyo sana na ari ya vijana waliyonayo na kama mlivyoona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, vijana hawa wamepikwa vizuri na wana ari, moyo na uzalendo mkubwa na kilicho mbele yao ni kitu kimoja tu, kupambana kufa au kupona na kurudi na medali,” alisema Mwakyembe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande, alisema kampuni yake ina dhamira endelevu ya kuibua na kuinua vipaji nchini na ndiyo sababu wakaamua kusaidia katika maandalizi ya timu. 

“Tumefadhili kwa kiasi kikubwa kambi ya timu iliyokuwa Ilboru Arusha na pia kuhakikisha kuwa timu inawasili Dar es Salaam na kujiandaa na safari ya London,” alisema Maharage na kuongeza kuwa wamekuwa wakimdhamini Balozi wao, Alphonce Simbu kwa mwaka mzima sasa.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa