Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SERIKALI IMEONYESHA MKAZO NA MSISITIZO KATIKA KILIMO CHA UMWAGILIAJI.

SERIKALI IMEONYESHA MKAZO NA MSISITIZO KATIKA KILIMO CHA UMWAGILIAJI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

KILIMO ndiyo Msingi wa Uchumi wa Taifa letu ambapo takribani asilimia 70 ya Watanzania hutegemea sekta hiyo kama shughuli kuu ya Kiuchumi.
 
Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba Nchi yetu ina eneo kubwa linalofaa kwa Kilimo takriban Hekta Milioni 29.4, ni Hekta 290,000 tu, sawa na Asilimia Moja (1%) zinazotumika kwa Kilimo cha Umwagiliaji Maji.

Kwa maana hiyo, Kilimo cha Umwagiliaji kinayo nafasi kubwa ya kuwezesha kufikia Mapinduzi ya Kijani kwa kuwa kinatuhakikishia uzalishaji endelevu wa mazao badala ya kutegemea mvua ambazo hazina uhakika wa kiasi na wakati wa kunyesha katika msimu.

Serikali imekusudia kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 1,000,000 katika skimu za wakulima wadogo, wa kati na wakubwa ifikapo mwaka 2020, ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza uzalishaji wa Mazao ya chakula na biashara na kuongeza tija katika kilimo.

Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge anasema hadi mwezi  Machi 2017, eneo linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 461,326 kwa mwaka 2015/2016 na kufikia hekta 468,338.

“Eneo hilo linachangia asilimia 24 ya mahitaji yote ya chakula nchini kwa sasa, ambapo hekta milioni 2.3 zina uwezekano mkubwa, hekta milioni 4.8 zina uwezekano wa kati na hekta milioni 22.3 zina uwezekano mdogo” anasema Mhandisi Lwenge.

Mhandisi Lwenge anasema katika mwaka 20176/18, Serikali inatarajia kutekeleza Mpango wa miaka 5 wa Programu ndogo ya Umwagiliaji iliyolenga katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika skimu na mabwawa ya umwagiliaji.

Waziri Lwenge anasema katika awamu hiyo, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika skimu 176, ukarabati wa skimu 205, ukarabati wa mabwawa 30 na kujenga mabwawa mapya 40 ili kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na matumizi mengine kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Mhandisi Lwenge anasema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wakulima na wataalam kuhusu usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji na kusajili vyama vipya 100 vya wamwagiliaji katika skimu za wakulima wadogo; na kuimarisha vyama 442 vya umwagiliaji vilivyopo.

Aidha Mhandisi Lwenge anasema Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuendeleza skimu za umwagiliaji za wakulima wadogo kwa awamu tatu katika Halmashauri 68 nchini.

Anasema kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2017, ukarabati na ujenzi wa skimu 45 za awamu ya kwanza umekamilika na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi unahusisha ujenzi na ukarabati wa skimu 63 ambapo ukarabati na ujenzi wa skimu 43 unaendelea; na taratibu za kuwapata Wakandarasi wa skimu 20 zilizobaki zinaendelea katika Halmashauri husika.

“Katika mwaka 2016/2017, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 32 imeendelea kusimamia ukarabati na uboreshaji wa skimu 45 za umwagiliaji za awamu ya kwanza zenye jumla ya hekta 13,722 na hivyo kumeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,326 hadi kufikia hekta 468,338” anasema Waziri Lwenge.

Serikali inaendelea kupitia Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo kazi hiyo inatarajia kukamilika katika mwaka 2018/2019.

Kukamilika kwa Mpango huo kutasaidia kuleta Mapinduzi ya Kijani nchini ambayo yanahitaji matumizi ya utaalamu, mbegu bora, mbolea, madawa, zana bora za kilimo pamoja na kuongeza eneo la Kilimo cha Umwagiliaji.

Aidha Mpango huo umekusudia kuweka mazingira mazuri ya kuongeza Uzalishaji katika Kilimo; kuongeza Pato la Mkulima; kupunguza Umaskini Vijijini na kushirikisha Sekta Binafsi kuleta uhakika wa Chakula katika Kaya.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa