Imeandikwa na Lucy Lyatuu
SERIKALI imesema kuanzia mwaka huu itatangaza kodi ambayo watu wote
wenye viwanja nchini, wakiwemo wanaoishi katika makazi yasiyopimwa,
wataanza kulipa kodi hiyo ya ardhi kwa kuhakikisha wananchi wote
wanaishi katika makazi yaliyorasimishwa.
Imesema wanaoishi katika makazi yasiyopimwa watatambuliwa kwa kupewa
leseni za makazi zitakazokuwa na ukomo, wakitakiwa kuishi kwa muda
utakaopangwa na baada ya kipindi hicho kumalizika, watatakiwa maeneo yao
yawe yameshapimwa tofauti na hivyo manispaa zitaagizwa kufunga nyumba
zao. Aidha, imesema serikali haitojihusisha tena katika kupima maeneo
yoyote ya ardhi kuanzia sasa, na badala yake kinachotakiwa ni wananchi
wenyewe kuwajibika kwa kuunda kamati za urasimishaji zitakazosaidia
maeneo yao kupimwa.
Kadhalika imesema katika kudhibiti matapeli wa ardhi, na migogoro
mbalimbali ya ardhi, inaanzisha mradi mpya utakaoanzia katika Manispaa
ya Ubungo na Kinondoni ambao utawezesha kutoa hati za makazi katika njia
ya elektroniki. Hata hivyo, imetoa hati 84 za makazi kwa wananchi wa
Kata ya Kimara, Mtaa wa Kilungule A Manispaa ya Ubungo jijini Dar es
Salaam na tayari viwanja 4,333 vimeshapimwa, ikiwa ni utekelezwaji wa
mpango darasa wa kupima viwanja 6,000 vya kata hiyo na mitaa yake sita.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi hati hizo kwa
wananchi wa Mtaa wa Kilungule na kuongeza kuwa wenye viwanja vikubwa
visivyopimwa nao watawajibika kulipa kodi na kuhakikisha maeneo hayo
yanapimwa.
“Maeneo yote yasiyopimwa ambayo ni makazi holela watapewa leseni na
baada ya muda fulani yatatakiwa kuwa yamepimwa,” alisema Lukuvi na
kuongeza kuwa ni lazima maeneo yote nchini yarasmishwe na kuanzia sasa
serikali haiwajibiki tena kupima na upimaji wa Kata ya Kimara ni wa
mwisho, wananchi wakitakiwa kushughulika wao wenyewe wakianza kuwa
kuunda Kamati za urasmishaji katika mitaa yao.
“Kamati hizo ni za wananchi wenyewe watakaoshughulika nazo, na fedha
watakazokuwa wakichanga zisiende halmashauri au wizarani kwani
zitaibiwa, wawe wenyewe na hata mtumishi wa serikali asiwe mtia saini,”
alisema Lukuvi na kuongeza kuwa wananchi wenyewe ndiyo watakaoamua nani
wamuweke wapi na watakaowaamini. Alisema nchi nzima ziundwe Kamati za
Urasmishaji zitakazokuwa na mpango madhubuti wa urasmishaji na serikali
itaingia kwa kupeleka wataalamu.
Kuhusu wenye viwanja vikubwa, waziri huyo alisema Dar es Salaam wapo
wananchi wenye maeneo mengi yasiyopimwa huku akiishi kwa kutambuliwa na
Serikali za Mitaa ambapo atatakiwa kuanza kulipa kodi. “Wapo watu wenye
ekari mpaka mia tatu wanakaa tu, akiuza kiwanja kimoja kimoja kila
mwaka, hakuna mtu atadumu na eneo kubwa mjini lisilopimwa na
lisilolipiwa kodi, maana wapo wanaotunza tu maeneo, hakuna shambabubu
mjini waende mikoani,” alieleza Lukuvi.
Alitolea mfano wenye maeneo makubwa eneo la Kigamboni kwamba watu wa
aina hiyo wanatakiwa kulipia kodi kubwa zaidi ili manispaa zipange
mipango yake ya mendeleo, kwa kuwa haiwezekani kuyashika tu maeneo.
Alizitaka manispaa zote kutoruhusu watu kujenga ovyo, wakitakiwa kuwa
macho na hata kama lipo eneo lililoko wazi walichukue na kulipima.
Kuhusu hati, alisema katika Jiji la Dar es Salaam eneo lisilopimwa ni
asilimia 75, hivyo wananchi wengi wamekuwa wakiishi katika makazi
yasiyopimwa na Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuwaondolea wananchi
urasimu ama kero za ardhi na watu waliojiona mangimeza. Alisema wananchi
walikwazwa na gharama za urasmishaji na tayari serikali imepunguza
umilikishaji wa ardhi kwa asilimia 67, tozo hiyo kwa sasa nchi nzima
itakuwa asilimia 2.5 na italipwa mara moja na baada ya mwananchi kupata
hati, tozo hiyo ni ya mara moja kwa mwaka.
Alisema katika kupunguza kero hizo za ardhi, wizara yake imezungumza
na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili
kupunguza urasimu na itapeleka muswada bungeni ili utoaji wa vibali vya
ujenzi katika manispaa upitishwe kwa haraka ndani ya wiki moja ili
wananchi wapate fursa ya kujenga kwa haraka huku vibali vikipatikana.
Aliwaonya viongozi wa mitaa kuacha kushirikiana na matapeli wakitumia
ovyo mihuri yao, kwamba wapo baadhi yao tabia zao ni za ovyo,
waliogombea nafasi hizo wakiwemo wasiokuwa na sifa lengo likiwa ni
kumiliki maeneo ya watu.
“Katika hili, wakuu wa wilaya fanyeni ukaguzi katika maeneo yenu
muone kama wananchi wenu walijenga ama wanamiliki kwa mujibu wa sheria,”
alisema Lukuvi na kuongeza kuwa wapo wenyeviti wa mitaa, watendaji
wenye ndoa za kudumu na matapeli jijini.
“Wengine wamekuwa wakijifanya mapredeshee mijini wakivaa cheni kubwa
kumbe ni wezi tu wa ardhi, nimeanza kutoa majina pale wizarani kwamba
hakuna kupokea muamala au nyaraka yoyote, ubadilisho wa hati yoyote
wakiona majina ya watu fulani fulani ambao ni matapeli, wako watu
niliwahi kuwahamisha Dar na ninasikia wamerudi nitachunguza na
nikigundua wamerudi nitawatupa Tanganyika,” alisema Lukuvi akisisitiza
kuwa Jiji la Dar es Salaam limeharibika sana na wananchi wakionewa sana.
Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Mipango Miji nchini, Profesa John
Lupala alisema mradi wa urasimishaji Kata ya Kimara ulikuwa ni mpango
darasa ili kujifunza na ulianza Januari mwaka jana na uandaaji ukianza
Aprili, 2016.
Profesa Lupala alisema mpango huo ulihusisha Kata ya Kimara na
Saranga kwa lengo kupima vipande 6,000, wakianza na urasmishaji, kufanya
uchambuzi, michoro ya mipango miji, upimaji na kumilikisha. Alisema
hadi Juni 30, 2017 wametambua vipande 4,768 na viwanja 4,333 vimepimwa
na vilivyobakia 1,607, mradi ukitekelezwa kwa asilimia 79.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment