Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » UCHUMI WA TANZANIA WAENDELEA KUIMARIKA-DKT. ABBASI

UCHUMI WA TANZANIA WAENDELEA KUIMARIKA-DKT. ABBASI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 





Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi nchini  Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Sehemu ya Habari na Picha Bw. Rodney Thadeus.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi (hayupo pichani) alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu hali ya uchumi mbele ya waandishi wa habari  Jijiji Dar es Salaam.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi akiwasilisha mada kuhusu hali ya uchumi wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari   Jijini Dar es Salaam.
Picha zote na: MAELEZO

By Bushiri Matenda-MAELEZO

Licha ya kuyumba kwa uchumi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani, Tanzania imeendelea kuongoza kwa ukuaji wa uchumi miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zimetaja uchumi wa Tanzania kuwa imara.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alibainisha hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya uchumi nchini.

“Uchumi wa Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo sasa bado uko katika ukuaji usiopungua asilimia 7.0 hadi 7.2 ikiwa ni ukuaji wa juu katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo Rwanda inakua kwa asilimia 6, Uganda asilimia 5 na Kenya asilimia 6.4”, alisema Dkt. Abbasi.

Alieleza kuwa sambamba na ukuaji wa uchumi, Tanzania imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo taarifa ya hivi karibuni zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kuwa mfumuko wa bei nchini umeshuka kutoka asilimia 6.1 mwezi Mei hadi kufikia asilimia 5.4 mwezi Juni mwaka huu.

Aidha, Mkurugenzi Dkt. Abbasi alieleza kuwa katika eneo la mazingira bora ya uwekezaji, Tanzania imeendelea kufanya vizuri ambapo alitoa takwimu za taasisi ya Quantum Global Research Lab ya Uingereza kuhusu Farihisi ya Uwekezaji Afrika ambazo zilionesha Tanzania ikiongoza miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki na ya nane Barani Afrika, ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.

“Mashirika ya Kimataifa kama IMF, Benki ya Dunia katika ripoti zao za hivi karibuni yamesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania ni imara na wamesifu mageuzi makubwa yanayofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli”, alieleza Dkt. Abbasi na kusema kuwa mashirika hayo yameitaka Serikali iendeleze mapambano zaidi dhidi rushwa na udhibiti wa mapato ya Serikali.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kufanyia kazi maoni hayo ya IMF na Benki ya Dunia na kwamba mabadiliko makubwa yamefanyika katika kupambana na rushwa na kudhibiti mapato ya Serikali ambapo ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 925 kwa mwaka 2015 hadi shilingi trilioni 1.069 kwa mwaka 2016/17 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.


Dkt. Abassi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alieleza kuwa kutokana na uchumi wa Tanzania kuwa imara kumeiwezesha Serikali kufanya maboresho makubwa katika sekta mbalimali zikiwemo afya, elimu, miundombinu na nishati ambapo katika sekta ya afya Serikali imetenga shilingi trilioni 1.077 kwa mwaka wa fedha 2017/18 kulinganisha na shilingi bilioni 796 zilizotengwa mwaka fedha 2016/17.

Alieleza kwa kwa upande dawa na vifaa tiba, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza ahadi yake kwa kuongeza fedha katika ununuzi wa dawa ambapo katika kipindi cha miaka mitatu fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba zimeongezea kutoaka shilingi bilioni 30 mwaka 2015/16 mpaka kufikia shilingi bilioni 261 katika bajeti ya mwaka 2017/18.

“Katika kuhakikisha Watanzania wengi wanaelimika, Serikali imeendelea kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne ambapo takribani shilingi bilioni 18 hutumika kwa mwezi na zinawafikia walengwa na kwa wakati”, alieleza Dkt. Abbasi na kuongeza kuwa wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kulikuwa na shilingi bilioni 341 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu lakini Rais John Pombe Magufuli akaongeza hadi kufikia shilingi bilioni 475 na kwa mwaka 2016/17 bajeti ya mikopo ya elimu juu iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 483.

Alieleza kuwa kutokana na uchumi imara, Tanzania imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo ikiwemo ile ya umeme, maji, reli ya kisasa, barabara na pia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda mapka Tanga nchini Tanzania, ambapo mradi huu unatekelezwa kwa pamoja na nchi hizo mbili.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa