Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Judith Mhina
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, anahitaji
kupata usaidizi wa kutosha kutoka kwa viongozi na hasa wasaidizi
kuanzia ngazi ya nyumba kumi hadi taifa.
Maneno hayo yametamkwa
na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba alipofanya mahojiano na
Idara ya Habari – MAELEZO ofisini kwake Oysterbay Jijini Dar-es-Salaam.
Jaji Warioba ameona kuna udhaifu mkubwa wa kiutendaji ambapo
wananchi hawatoi changamoto zinazowakabili mpaka wamuone Rais amefika
katika eneo lao, au wanaeleza changamoto zinazowakabili kwa viongozi
husika ila, viongozi hawazifanyii kazi, ambapo wananchi wanaamua
kuziwasilisha kwa Rais mara wanapomuona.
“Rais hawezi kufanya
kazi peke yake naomba tuimarishe utendaji wetu wa kazi, kama utendaji
ungekuwa mzuri suala la makontena kufika hadi bandarini lisingekuwepo,
na hata kugundulika kwake kusingefanywa na Rais,” amesema Jaji Warioba.
“Nampongeza
sana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia
Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa utendaji wao wa
kazi. Viongozi hawa ni wasikivu na wanatekeleza kazi zao bila mihemko
kwa kutoa maagizo na maelekezo kwa wahusika ili wayatekeleze”. Aliongeza
Warioba.
Hivi karibuni, Rais ameona tatizo hilo, la kuachiwa
kila jambo ili afanye wakati kuna uongozi wa serikali, kuanzia ngazi ya
nyumba kumi hadi taifa. Rais amelisema hilo, alipokuwa kwenye ziara
katika Mkoa wa Tabora, ambapo mabango mengi yaliyoandikwa na wananchi
yakiwa na changamoto mbalimbali na kugundua kuwa viongozi walio wengi
hawatatui changamoto hizo. Matokeo yake, Rais anapofika eneo husika,
kila mwananchi anataka atatuliwe changamoto yake kitu ambacho
hakiwezekani na wala sio sahihi.
Tabia hii haikumpendeza Rais
Magufuli, ambapo alipotoa kauli kuwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi
wa Halmashauri na watendaji wengine ambao hawatatui matatizo ya
wananchi atawaondoa katika nafasi hizo mara moja.
“Endapo
nitarudi na kuelezwa kero ambazo mnaweza kuzitatua lakini mkashindwa
kufanya hivyo, nitajua kuwa mmeshindwa kufanya kazi yenu kwa ufanisi”
alisema Rais Magufuli.
Warioba ameongeza kwa kusema; “Sisi wote
tulikuwa viongozi lakini hatukuwahi kuachiwa tufanye kila kitu bila
usaidizi wa viongozi katika ngazi zote.
Tanzania ni kati ya nchi
zilizojizatiti kwa kuwa na uongozi kuanzia ngazi ya nyumba kumi, shina,
kata, tarafa, Wilaya, Mkoa hadi taifa. Kama kweli uongozi wa kila ngazi
utajituma kutatua changamoto za wananchi itamrahisishia Rais kufanya
majukumu yake.
Mtakumbuka kuwa enzi za awamu ya kwanza na ya
pili, sio kweli kwamba hali ilivyo sasa ni mbaya kuliko awamu hizo.
Lakini wakati ule kilichotusaidia ni umoja wetu na mshikamano wa kutatua
matatizo yetu kwa pamoja, hatukuachiwa kama viongozi tutatue changamoto
za wananchi sisi wenyewe. Amesema Warioba.
Akisisitiza, Warioba
amesema; “Iweje leo tumuachie Rais afanye kila kitu mwenyewe naomba sana
tumsaidie na kumuunga mkono, hakika ana nia njema na rasilimali za nchi
hii. Ni vema kilichofanyika kikaangalia rasilimali zote za nchini na
sio wawekezaji wa nje tu hata wa ndani”.
Aidha, kiongozi mwingine
aliyeliona tatizo hili ni Waziri Mkuu Msataafu Dkt. Salim Ahmed Salim,
ambaye amesema Vijana ni lazima wajue siasa za nchi yao na nini muelekeo
wa uongozi wa nchi kwa ujumla. Uongozi ni dhamana unayopewa kwa niaba
ya wananchi wa Tanzania, hivyo ni lazima uwatumikie ikiwa ni pamoja na
kutatua changamoto zinazowakabili.
“Bila kujua historia na siasa
ya nchi yako utashindwa kuwatumikia wananchi badala yake utafanya kazi
kwa matakwa yako, ambapo itakuwa sio sahihi. Wito wangu viongozi wote
msaidieni Rais katika kutimiza wajibu wa Watanzania, msimuache afanye
kazi peke yake, sisi sote tumuunge mkono”Amesema Dkt. Salim.
Tangu
Rais ateue viongozi mbalimbali ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa,
kila kiongozi anajua utendaji wa Rais na nini anataka wafanye. Viongozi
wameapa na kupewa miongozo ya utendaji wa kazi zao. Kutokana na Rais
kuwa wazi katika hilo nadhani sasa kila mhusika atafanya ipasavyo ili
kutatua changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi.
Mfano mzuri ni
ule uliotolewa na Kamati ya maridhiano ya viongozi wa madhehebu ya dini
Tanzania ya kuomba viongozi wengine kuiga utendaji wa Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, ambaye walimpongeza
kwa kutatua kero za ardhi kila mahala hapa nchini. Kiongozi huyo
amejitahidi kupunguza
kero za watumishi wa ardhi wasio waaminifu
kwa kudai rushwa, katika suala zima la kupata viwanja, kupima na kupata
hati miliki.
Hivyo, kila mhusika katika Mkoa, Wilaya, Tarafa,
Kata, shina na nyumba kumi anawajibu wa kutatua kero na changamoto
zinazowakabili wananchi wa eneo lake. Iwapo kero ipo nje ya uwezo wa
uongozi wako, utashirikiana na ngazi iliyokuzidi kuhakikisha unaipeleka
mbele zaidi itatuliwe na kuchukuliwa hatua zinazofaa.
Kiongozi
hutumia busara, badala ya kusubiri Rais afike katika eneo lake na
wananchi waanze kulalamika, tafsiri yake ni kwamba hufai kuwepo kwenye
nafasi husika, hivyo ni vema ukatafuta kazi nyingine ya kufanya.
Baba
wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliona tatizo hili
la wananchi na viongozi wote kuwa ni sehemu ya kulalamika badala ya
kutafuta jinsi ya kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili kwa wakati
huo baada ya uhuru.
Mwalimu akaliona kama donda ndugu ambalo
likiachwa litaambukiza kizazi na kizazi, hivyo alitafuta dawa na kuja
na waraka wa serikali wa kusema “Toa Hoja usipige kelele” akiwa na maana
hoja yako itaangaliwa, litafanyiwa kazi na kutolewa majibu , lakini kwa
kupiga kelele watu wanaweza kudhani wewe ni mwendawazimu tu na
wakakupuuza na tatizo litabaki palepale.
Mpaka sasa Waraka
huu wa Mwalimu Nyerere alioutoa mwaka 1964 una umuhimu na mantiki ya
hali ya juu. Watanzania tutoe hoja tusipige kelele.
0 comments:
Post a Comment