Imeandikwa na Halima Mlacha
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha rasmi mfumo
mpya wa kulipia kodi ya ardhi kwa njia ya kieletroniki, unaolenga
kupunguza kero wanazopata walipa kodi ya kutumia muda na mlolongo mrefu
wakati wa kulipia.
Kuanzia sasa mmiliki yeyote mwenye ardhi iliyopimwa na kupatiwa hati
ya umiliki, anaweza kuulizia kiasi cha fedha anazodaiwa na kulipia kodi
hiyo ya mwaka kwa kutumia simu yake ya mkononi, tovuti ya wizara hiyo au
kulipia kupitia benki. Pamoja na hayo, wizara hiyo, imepanga
kushirikiana na serikali za mitaa kufanya ukaguzi maalumu wa maeneo yote
ya ardhi yasiyopimwa, ili kuweza kujua ni wananchi wangapi wana maeneo
hayo na maeneo gani, waweze kuingizwa kwenye mfumo wa kulipia kodi ya
ardhi.
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusikula
alisema mfumo huo utamuwezesha mmiliki wa ardhi kulipia ardhi hiyo kwa
dakika chache, badala ya kutumia siku nzima kusubiri kupata huduma ya
malipo.
“Zamani watu walikuwa wanatumia muda mwingi kufanikisha kulipia kodi
ya ardhi, walilazimika kwenda kwenye vituo vyetu aulizie kwanza deni
lake ndipo alipie, wakati wote huo hulazimika kupanga foleni ndefu kwa
kuwa watu ni wengi wanaolipia huduma hiyo.
Sasa tumekuja na mfumo huu kwa ajili ya kuwarahisishia wananchi,”
alifafanua. Alisema wizara hiyo imeingia mkataba na kampuni tatu za simu
za mkononi zinazotumia huduma za fedha kwa njia ya mtandao ambazo ni
Tigo, Vodacom na Halotel, lakini pia imeingia mkataba na benki mbili za
NMB na CRDB kwa ajili ya huduma hizo za malipo ya kodi ya ardhi.
Alisema katika huduma hiyo ya eletroniki kila muamala utakuwa na
risiti ya eletroniki, lakini pia endapo mmiliki wa ardhi atahitaji
risiti za kawaida, atawasilisha kwenye vituo vya ardhi au wizarani
ujumbe mfupi wa kukamilisha malipo na kupatiwa risiti yake. Hata hivyo,
alisema changamoto inayoikabili mfumo huo kwa sasa ni elimu kwa wananchi
kwani wengi wao bado hawajaelewa vyema namna mfumo unavyotumika hasa
katika kulipia kodi hiyo.
Alisema kutokana na hali hiyo, wizara hiyo imepanga mwezi wote wa
Agosti mwaka huu kupeleka wataalamu wake katika kila halmashauri kwa
ajili ya kutoa mafunzo juu ya namna sahihi ya kutumia mfumo kwa
wananchi. “Napenda kubainisha kuwa, zamani tulikuwa na akaunti za
kukusanyia kodi hii, lakini sasa tunazifunga akaunti zote na kuachia
mfumo huu wa eletroniki ndiyo uhusike na malipo ya kodi hii,” alieleza.
Akizumgumzia maeneo yasiyopimwa, Dk Kusiluka alikiri kuwa kwa sasa
maeneo hayo hayapo kwenye mfumo huo wa elektroniki, lakini baada ya
kufanya ukaguzi maalumu yataingizwa kwenye mfumo wa kulipia kodi hiyo,
wakati utaratibu wa kupima ardhi ukiendelea nchi nzima.
Aliwatahadharisha wale wote wanaomiliki ardhi na kuwa na hati au ofa,
kuhakikisha wanalipia kodi hiyo kwa wakati, vinginevyo muda wa malipo
ukipita watatozwa faini na wasipolipa pia baada ya siku 14 wataburuzwa
mahakamani. Kwa mujibu wa mfumo huo, wanaotumia mitandao ya simu
wanatakiwa kupiga namba *152*00# na kufuata maelekezo, na kwa wale
wanaotumia mtandao wa wizara waingie kwenye tovuti www.ardhi.go.tz.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment