Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » WANAOJIPENYEZA BARABARA ZA MWENDOKASI WADHIBITIWE

WANAOJIPENYEZA BARABARA ZA MWENDOKASI WADHIBITIWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


MABASI yaendayo haraka yalianza kazi rasmi kusafirisha abiria Mei 10 mwaka jana yakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo mabasi hayo kugongwa kwa kuingiliwa kwenye barabara zake.

Watuhumiwa wakubwa wa uhalifu huo ni madereva wa pikipiki, maarufu kama 'bodaboda' na magari, waliokuwa wakilazimisha kupita kwenye barabara maalum za mabasi hayo huku wakitambua kuwa hawaruhusiwi.

Kutokana na ubishi huo, kuna waliofariki dunia kwa kugongwa na mabasi hayo au kupata vilema vya kudumu.

Baada ya kipindi kadhaa sasa angalau wahusika wameanza kuzingatia sheria za usalama barabarani huku wengine wakiendelea kuwa wagumu.

Kuna baadhi ya madereva ving'ang'anizi wanaendelea kupita kwenye barabara za mabasi hayo, hali inayoonyesha kuwa, bado kuna haja ya wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Ikumbukwe kuwa, mabasi hayo yanatumia barabara zilizojengwa kwa gharama kubwa, lengo ni kupunguza kero ya foleni za magari inayosababisha watu kuchelewa kwenye shughuli zao za kila siku.

Nakumbuka mabasi hayo yalipoanza kazi, askari wa manispaa ya Kinondoni walikuwa wakiwacharaza bakora baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwa wakikaidi kwa kuacha njia zao na kupita kwenye barabara za mabasi hayo.

Binafsi sikuona ubaya wowote kwa hatua hiyo, kwani ililenga kusaidia kuokoa maisha yao.Lakini bahati mbaya sheria hairuhusu, ndiyo maana wakazuiwa kuwashughulikia wabishi hao kwa njia ya bakora.

Lakini kama ungekuwa ni uamuzi wangu. Yawezekana adhabu hiyo kwa namna moja ama nyingine ingesaidia kuwaweka sawa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kama ni elimu imetolewa sana kuhusu matumizi ya barabara hizo, lakini bado wanakaidi !

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli naye alionyesha kukerwa na watu hao hata kuagiza wakamatwe na kufikishwa kwenye mamlaka husika kwa sababu ya kuvunja sheria makusudi. 

Ninaunga mkono kauli hiyo ya rais, kwa sababu haiingii akilini kuona mwendesha bodaboda anaacha barabara za pembeni kisha anajipenyeza katikati kufuata mabasi ya mwendo wa haraka. Huko anatafuta nini?

Inashangaza kuona, serikali inajitahidi kukabili kero ya usafiri, lakini wanaibuka wachache wanaanza kukwamisha jitihada hizo. Hawa ni watu wa kushughulikiwa ili mwishowe wataheshimu sheria.

Ilifikia hadi kuharibu vituo vya kupumzikia abiria, kugonga kingo za barabara na taa ingawa kwa sasa matukio hayo ni kama yamepungua. Hata hivyo ni vyema kuwa na ufuatiliaji wa kila mara.

Ninasema hivyo kwa sababu, licha ya uharibifu huo, ulikuwa umeibuka mwingine wa baadhi ya watu kugeuza madaraja ya Ubungo, Kimara na Morocco kuwa sehemu ya kujisaidia haja kubwa na ndogo na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Mtindo huu wa kuharibu na kuchafua miundombinu hii, ni muhimu ufuatiliwe ili usijirudie, kwa sababu binadamu wana kawaida ya kujaribu.

Wanaweza kuona kimya wakarudia tena mtindo huo, ambao kwa kweli siyo wa kistaarabu hasa kwa watu wanaoishi mjini, ambao wanatarajiwa kuwa kama kioo kwa wanaoingia mjini.
Nina uhakika kwamba, wakibanwa wataheshimu sheria na kuachana na mtindo wa kupita kwenye barabara wasizoruhusiwa. Pia hatawaharibu au kuchafua miundombinu ya barabara hizo.

Ubishi wa kutotii taratibu, kanuni na sheria usipoachwa unaweza kuleta madhara kwa wahusika na wasiohuka, hivyo njia pekee ni kutii sheria bila kusubiri kusukumwa.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa