Imeandikwa na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi nchini limewataka Watanzania kutoa ushirikiano
kuwapata wahusika wa kikundi cha vikoba kiitwacho Focus Vicoba Tanzania
kwa kuwa ni cha kitapeli.
Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa, alisema katika taarifa
yake kwa vyombo vya habari jana kuwa, kikundi hicho kinatumia majina ya
viongozi ikiwemo Mama Salma Kikwete, kufanya utapeli.
“Katika siku za karibuni kumejitokeza vitendo vya baadhi ya watu
kutumia majina ya viongozi ama wake wa viongozi wa nchi kufanya utapeli
unaohusisha wizi wa fedha kwa njia ya mtandao,” alisema Mwakalukwa.
Alisema uchunguzi wa jeshi hilo umebaini uwepo wa kikundi cha Focus
Vicoba Tanzania ambacho kinatangaza kuwa kipo chini ya uongozi wa Mama
Salma Kikwete (mke wa Rais Mtaafu, Jakaya Kikwete, sasa Mbunge),
kuwatapeli watu kuwa kinatoa mikopo kwa wanachama wanaojiunga nacho.
Alisema Polisi inatoa mwito kwa wote waliotapeliwa na kikundi hicho
kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), au
Kamanda wa Polisi Mkoa, ama katika Kituo cha Polisi chochote cha karibu
ili kutoa ushirikiano kwa ajili ya taratibu za kiuchunguzi kuwabaini
wahusika.Awali kikundi hicho kiliwahi kuripotiwa kikijitangaza kuwa
kinamilikiwa na Mkurugenzi wa Kampuni za IPP kwa utapeli kama huo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment