na Nasra Abdallah
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinatarajia kuongeza udahili wa wanafunzi katika fani ya uvuvi na uchumi ili kuongeza idadai ya wataalamu katika sekta hiyo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Makamu Mkuu wa wa chuo hicho, Yunusi Mgaya, wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa uvuvi uliofanyika kwa siku nne jijini Dar es Salaam.
Mgaya alisema pamoja na sekta hiyo kuwa muhimu katika kuchangia pato la taifa lakini wamegundua kuwa kuna uhaba wa wataalamu wa fani hiyo, hivyo kazi hiyo kufanywa kienyeji zaidi.
Kwa mujibu wa Mgaya mpaka sasa ni vyuo viwili tu vinavyotoa taaluma hiyo ambavyo ni UDSM na Sokoine, jambo ambalo linahitaji jitihada zaidi za kuongeza wanafunzi watakaochukua fani hiyo.
Pia alisema wamedhamiria kuwa na tafiti nyingi zaidi katika sekta ya uvuvi ili ziweze kuja kusaidia vizazi vilivyopo na vijavyo na kuhakikisha sekta hiyo inachangia uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Visiwani Zanzibar, Abdillah Jihad Hassan, alisema bahari ni sawa na ardhi hivyo inapaswa kulindwa mazingira yake kwa hali ya juu.
Hassan alisema njia zinazotumika kwa sasa katika kuvua zinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, hivyo kusababisha kuua mazalia ya samaki na viumbe wengine wa majini.
“Ili kuhakikisha bahari inakuwa salama ni wajibu wa serikali na watu binafasi kuhakikisha tunapeana elimu ya uvuvi na mazingira ya bahari kwa kuwa kuna njia nyingi mbadala ambazo tunaweza kuzitumia katika kuvua ambazo haziitaji uwekezajki mkubwa,” alisema waziri huyo.
Mkutano huo wa uvuvi ulishirikisha takriban wajumbe 250 kutoka nchi mbalimbali duniani, ambapo Tanzania imekuwa ya kwanza kuwa mwenyeji kwa nchi zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment