na Asha Bani
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki amesema kuwa idadi ya watalii wanaoingia nchini ni ndogo, pia inatia aibu licha ya kuwapo vivutio vya kutosha ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.
Kagasheki aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, jana katika ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mashirika Yanahusika na Masuala ya Utalii (TCT).
Alisema idadi ya watalii kwa mwaka, ni laki nane ukilinganisha na nchi ya Kenya ambayo ni milioni 1.4 na Zimbabwe milioni 2.4 jambo ambalo linashangaza kutokana na Tanzania kuwa na vivutio vingi vya utalii kuliko nchi hizo.
Waziri huyo alisema kwa hali hiyo, kuna haja ya serikali kukaa na wadau wa masuala ya utalii kuzungumza nao ili kukusanya maoni yao kubaini matatizo yaliyopo katika sekta hiyo.
Alisema, hata hivyo serikali itafanya marekebisho ya sheria mbalimbali zilizopitwa na wakati ili kuiwezesha sekta hiyo kujipambanua kufikia lengo la kupata watalii zaidi ya milioni moja ifikapo mwakani.
Kagasheki alisema sekta hiyo ikisimamiwa vema itachangia pato la taifa, kwa kupata fedha nyingi za kigeni kama ilivyokuwa hapo awali.
“Utalii inachangia asilimia 26 fedha za kigeni na kwa kuchangia pato la taifa, ni ya pili huku ya kwanza ikiwa madini, lakini hapo awali maliasili ilikuwa ya kwanza. Sasa kuna haja ya kuisimamia vema, kutangaza utalii wake ndani na nje ya nchi ili iweze kuwa namba moja kama hapo awali,” alisema Kagasheki.
Mkutano huo uliwashirikisha wawindaji wa kitalii, wamiliki wa mahoteli, waongoza watalii pamoja na utalii wa asili.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment