Tuesday, August 7, 2012

KAMPUNI INAYOIHUJUMU TANESCO YANASWA DAR, INAUZA LUKU, KUFUNGA MITA, KUTENGENEZA UMEME KWA BEI POA

na Irene Mark
KAULI ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo kwamba kuna vigogo wanaoshirikiana na wafanyakazi wa Shirika la Umeme (TANESCO), kulihujumu shirika hilo, imethibitika.
Jana, TANESCO iliinasa kampuni hewa inayotoa huduma sawa na shirika hilo na kulisababishia hasara ya mabilioni ya shilingi kwa miaka saba sasa.
Kampuni hiyo yenye makazi yake Mwananyamala barabara ya Mwinjuma jijini Dar es Salaam, ilisajiliwa kwa jina la Low Voltage Distribution ambayo mmiliki wake ni Mussa Mtavazi, ilibainika jana baada ya watendaji wa TANESCO na maofisa wa polisi kuvamia eneo hilo.
Kampuni hiyo ipo kwenye nyumba namba 648 mali ya Bakari Issa aliyeeleza kwamba mkataba wa upangaji kwenye nyumba hiyo, uliwekwa kati yake na Mtavazi kwa makubaliano ya kulipa pango la sh 25,000 kwa mwezi malipo yanayofanyika kila baada ya miezi minne.
Zoezi la kumnasa mmiliki huyo mwenye ‘TANESCO’ ndogo lilifanikiwa jana saa saba mchana wakati watendaji wake wakiwa kazini kama kawaida ghafla maofisa wa polisi kutoka kituo cha Oysterbay waliokuwa na hati ya upekuzi, watumishi wa TANESCO na waandishi wa habari walipovamia nyumba hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi hiyo muda mfupi baada ya kukamatwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Low Voltage Distribution, Ibrahim Said alikiri kwamba kampuni hiyo inafanya shughuli zote za TANESCO ikiwemo kuuza luku, kufunga mita kwa wateja, kutengeneza umeme na shughuli nyingine.
Hata hivyo, ndani ya ofisi hiyo kulibainika kuwepo kwa sare za watumishi wa TANESCO, mita za umeme na vifungio vya mita (Seal), mikanda na ngazi za shirika hilo inayotumika kupanda kwenye nguzo, tokeni za luku, kufunga umeme majumbani na mafaili yenye namba za wateja.
Kwa upande wake Meneja Habari na Mawasiliano wa TANESCO, Badra Masoud alisema kazi hiyo ni sehemu ya maboresho ya utendaji wa shirika hilo huku akiwataka wote wanaolihujumu kuacha vinginevyo mkono wa sheria utawafikia.
“Tunajua kwamba shirika linahujumiwa tena tunaamini wanaolihujumu sio watu kutoka mbali, wapo humu humu ndani ni watumishi wenzetu wanaoshirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Hivi vitu zikiwemo sare za TANESCO tulizozikuta kwenye hii kampuni vinagharama kubwa kuvipata, lakini yeye anavimiliki isivyo halali… ameiba channel (njia) ya luku na anawauzia wafanyabiashara wengine kinyume cha sheria, mapato hayatufikii.
“Ukija hapa kununua luku unaipata kwa bei nafuu sana halafu sasa hizo pesa anabaki nazo huu ni wizi kwa shirika, tunajua kwa miaka hiyo saba amewauzia watu wengi na sisi tutawafuatilia mmoja baada ya mwingine na kuwanasa.
“Nawashauri wote wanaoliibia shirika kujisalimisha… tukimgundua sheria inachukua mkondo wake, hakuna msalie mtume katika hili,” alisema Badra huku akiwaonyesha waandishi wa habari baadhi ya vifaa vya TANESCO vilivyokutwa kwenye ofisi hiyo.
Kwa mujibu wa Badra, shirika litafanya tathimini ya hasara na gharama ya mali zilizokutwa kwenye ofisi hiyo ili kujua gharama halisi huku watendaji wake wakiendelea kuwatafuta wananchi wengine wanaoshiriki kulihujumu shirika huku akisisitiza kwamba wahujumu wote watachukuliwa hatua za kisheria.
Hivi karibuni akiwa bungeni, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo aliwataja baadhi ya watu, Taasisi na Makampuni yanayoshiriki kulihujumu shirika la umeme akiwemo Mbunge wa Viti Maalum, Getrude Lwakatare kupitia shule zake za St. Mary’s.
Profesa Muhongo alisema, hadi sasa TANESCO imewabaini wezi wakubwa wa umeme wapatao 50 na kwamba kazi hiyo itaendelea ili kuhakikisha shirika hilo linaweza kujihudumia bila madeni makubwa na kutoa huduma bora kwa wateja wake.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment