Saturday, August 4, 2012

KIGAMBONI WAPINGA UJENZI MJI MPYA

Na Bakari Kimwanga, Dar es Salaam
SAKATA la ujenzi wa Mji mpya wa Kigamboni, limezidi kuchukua sura mpya, baada ya wakazi wake kuapa kumwaga damu wakitetea ardhi yao kutokana na mradi huo kutofuata sheria kwa kuwashirikisha wananchi.

Mbali na hatua hiyo, wakazi hao wamesema endapo Serikali italazimisha kutekeleza mradi huo kwa kutumia nguvu, watahakikisha wanaiburuza katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague, nchini Uholanzi kwa kuvunja haki za binadamu.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, wakazi hao walipinga hatua ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kushirikiana na baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Temeke, kuendesha kampeni ya kujenga mji huo.

Akizungumzia suala hilo, kwa niaba wakazi wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wana Kigamboni, Kassim Abdallah alisema anashangazwa na hatua ya madiwani kutoa tamko kila wakati, ingawa hata siku moja hawajawahi kuwashirikisha wananchi.

“Kwa mujibu wa sheria ya Ardhi Namba 3, imeeleza wazi namna wananchi wanavyotakiwa kushirikishwa katika suala la ardhi yao, tunatambua kuwa ardhi ni mali ya Serikali, lakini si kwa hili wanalolifanya hawa madiwani pasi na kutumwa na mtu.

“Kwa hatua hii, tupo tayari kupoteza mali na uhai wetu kupigania haki yetu na hata ikiwezekana tutamwaga damu. Tunajua mradi huu upo kisheria, lakini tunalopinga ni namna mradi huu ulivyoghubikwa na rushwa ya hali ya juu kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi na baadhi ya madiwani.

Kwa upande wake, Ustadhi Ahmad Abdurahman, alisema Juni mwaka huu, walifanya mkutano na mbunge wao Dk. Faustine Ndugulile, katika uwanja wa Swala, ambapo wananchi walimweleza namna ukiukwaji wa sheria ulivyofanywa katika utekelezaji wa mradi wa mji mpya.

Naye Mwarami Mwinyimvua, mkazi wa Vijimbweni alisema hatua ambayo imefikia, wananchi hawatakuwa tayari kuona wanafanyiwa ujanja katika mradi huo.

Naye Exaud Mmari, alisema wananchi wa eneo hilo ni waelewa na walio wengi akiwemo yeye anatambua vizuri sheria za nchi hivyo Serikali inatakiwa kutambua kuwa wapo makini na kutumia nafasi hiyo kuweka wazi suala la haki halina chama cha kiasa na kushangazwa na madiwani wa CCM wanaokuwa mstari wa mbele kumchafua mbunge, aliyeaminiwa na wananchi wote kwa kutetea maslahi yao.

Katika mkutamo huo, wakazi hao walitumia nafasi hiyo kufafanua kuwa mji huo wa Kigamboni, ulipimwa mwaka 1952 na kuwa ni mji wa pili kupimwa, baada ya Magomeni huku wakiitaka Serikali kutambua kuwa wananchi hawapo tayari kuburuzwa katika mradi huo.
Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment