Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini Mohammed Mpinga, akiwa amepanda pikipiki akiashiria kuzinduliwa kwa mafunzo ya waendesha pikipiki 1000 watakaofunzwa bure kwa udhamini wa kampuni ya Automobile Association Tanzania.
Kamanda mpinga akifafanua jambo mbele ya wanahabari wakati wa uzinduzi huo leo asubuhi jijini.
Rais wa AAT Nizar Jivani, akifafanua jambo mbele ya wanahabari katika ukumbi wa idara ya habari MAELEZO leo asubuhi wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya waendesha pikipiki jijini.
Na Hafidh Kido
Kamanda wa polisi kitengo cha usalama barabarani nchini Mohammed Mpinga, amesema kwa miaka mine tangu pikipiki kuruhusiwa kubeba abiria kumekuwa na ongezeko kubwa la uingizwaji wa pikipiki kuliko magari.
Mpinga amesema hayo leo wakati akizindua mradi wa mafunzo ya waendesha pikipiki na bajaj jijini Dar es Salaam unaofadhiliwa na kampuni ya Automobile Association of Tanzania ambapo mradi huo utanufaisha waendesha pikipiki 1000 wa jijini watakaopata mafunzo bure kwa kipindi cha miezi sita.
“Tangu Serikali iridhie pikipiki hizi kubeba abiria kibiashara mwaka 2009, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la pikipiki hizi. Katika kipindi cha miaka mitatu yaani 2009-2011 jumla ya pikipiki 330,882 zilisajiliwa kati ya magari yote 561,190 ikiwa ni asilimia 60.
“Aidha mwaka 2011 pikipiki ziliongezeka kutoka 43,746 mpaka 85,702 mwaka 2009 ikiwa ni ongezeko la asilimia 51 na bajaj nazo ziliongezeka kutoka bajaj 2,124 mpaka 3,259,” alisema.
Akieleza changamoto wanazokutana nazo kwa ongezeko la pikipiki nchini kamanda Mpinga alisema ongezeko hili limeongeza idadi ya ajali za pikipiki, wizi na majeruhi wa pikipiki kwa waendeshaji na abiria.
“Aidha kwa upande wa ajali kwa kipindi cha miezi mitatu (April, May na June) 2012 jumla ya ajali za pikipiki 1,386 zilitokea na kusababisha vifo vya watu 251 na majeruhi 1,289,” aliongeza.
Kampuni ya AAT inayoshughulika na vyombo vya usafiri itagharamia mafunzo ya waendesha pikipiki 1000 katika jiji la Dar es Salaam na kuhakikisha kupunguza tatizo la madereva wasio na uzoefu ambao mara ningi ndiwo wanaosababisha ajali.
Akizungumzia mafunzo hayo Rais wa AAT Nizar Jivan anasema ‘tumeamua kupunguza ajali za pikipiki kwa kufungua mafunzo haya yatakayodumu kwa miezi sita, tutachukua madereva 30 kila wilaya Temeke, Ilala na Kinondoni. Halafu tutawaachia polisi kuangalia juu ya utaratibu.
“Kitu kinachohitajika ni mtu awe na umri usiopungua miaka 18, awe na leseni ya kuendesha bodaboda, na hata wasio na leseni pia wanaweza kujitokeza. Maana lengo letu ni kusaidia vijana, mafunzo haya yatakuwa bure bila malipo,” alieleza.
Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka ambapo vifo na ulemavu unaosababishwa na ajali za pikipiki nchini vimeshamiri, hivyo jeshi la polisi kuonekana kuelemewa na suala hili maana kila mtu anataka kufanya biashara hii ya pikipiki ili kujipatia senti.
Hata kama mtu hana ujuzi wa kuendesha pikipiki atajifunza usiku mmoja na siku ya pili anapita barabarani na kupishana na magari makubwa hali hana ujuzi wala elimu ya kukaa barabarani na chombo cha moto.
Chanzo: KIDOJEMBE
No comments:
Post a Comment