Friday, August 3, 2012

Mwanafunzi amchoma kisu mwalimu wake




Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Mbondole, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Neneu Baltazar, anatuhumiwa kuchoma kisu mwalimu wake, Frank Gama, baada ya kuzuka vurugu shuleni hapo.



Vurugu hizo zilitokea baada ya mwanafunzi wa kike kuibiwa simu yake ya kiganjani na kumhisi mwanafunzi mwenzake Neneu kuwa ndiye aliyehusika na wizi huo.

Hata hivyo, Neneu alipokataa, ndipo vurugu zilipoibuka kati ya wanafunzi hao wawili.

Akisimulia mkasa huo, Mwalimu Gama alisema baada ya kuona wanafunzi hao wanagombana, alichukua jukumu la kwenda kuamulia ugomvi huo.

Hata hivyo, alisema wakati akifanya hivyo, ghafla alijikuta akichomwa kisu mgongoni.

“Vijana hao wamenipiga sana lakini isingekuwa walimu wenzangu kuja kuniokoa, sijui ingekuwaje. Kwani walikuja kama nyuki nimeumizwa na sasa nakwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kutibiwa,” alisema Mwalimu Gama.

Makamu wa Mkuu wa shule hiyo, Juma Robinson, aliliambia NIPASHE jana kuwa vurungu hizo zilisababishwa na utovu wa nidhamu wa wanafunzi wa shule hiyo.

Alisema vurugu kama hizo za kupigwa walimu shuleni hapo, ni jambo la kawaida kwani hata yeye aliwahi kupigwa ngumi lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Hata hivyo, Juma alisema tukio hilo la jana walitoa taarifa  polisi jamii wa mtaa huo ambao walifika na kumkamata mmoja wa wanafunzi hao lakini wengine walikimbia. 

“Utovu wa nidhamu katika shule za kata zinasababishwa na kutokuwa na bodi za shule na maamuzi katika kila shule huachiwa mtu mmoja," alisema. 

Kamanda wa Polisi Jamii katika mtaa huo, Richard Mosoba, alisema walipofika eneo hilo, walimkamata mwanafunzi huyo na kumfikisha katika kituo cha  Polisi cha Stakishari Ukonga.

“Sisi tulijitahidi kutimiza jukumu letu la kumfikisha mtuhumiwa aliyemchoma kisu mwalimu, lakini nini kitafuatia, hiyo ni kazi ya polisi. Kwanza hatuna silaha zaidi ya pingu, sasa unategemea nini kitokee kwenye vurugu?,” Alihoji Mosoba.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ilala, Marietha Minandi, alithibisha kutokea kwa tukio hilo.

Alifafanua kuwa ugomvi huo uliwahusu wanafunzi na kidato cha tatu na cha nne baada ya mwanafunzi mmoja kuibiwa simu na kumhisi wa kidato cha nne kuwa ndiye aliyeiba.

Alisema wanafunzi walipigana na baadhi yao wakamua kumuita mwalimu aende kuwaamulia lakini alipofika mwanafunzi mmoja alichoma kisu.

Mwanafunzi huyo kwa sasa anamshikiliwa polisi kwa kwa mahojiano.

CHANZO: KULIKONI

No comments:

Post a Comment