Thursday, August 9, 2012

MWANAMKE AJINYONGA KWA KAMBA YA MANILA

Sebastian Mparazo na Sila Mnyawami

WATU watatu wamefariki dunia katika matukio matatu tofauti jijini Dar es salaam, likiwamo la mwanamke mmoja aliyejinyonga kwa kamba ya manila.

Tukio hilo lilitokea eneo la Chanika, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam ambapo mwanamke huyo alitambuliwa kwa jina la Fatuma Athumani (40) aliyekutwa amefariki chumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta Komba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu aliacha ujumbe wa maandishi uliosomeka.

“Namdai baba mkwe matofali 1900 alipe, nimechanganyikiwa, mwanangu hana kazi, sitaki wanangu waende kulelewa upande wa kiumeni.

“Waangalieni upande wa ndugu zangu, baba mdogo uza nyumba wapate mahala pa kukaa, bonge kachukua hela nyingi shilingi 1,000,000 peke yake,” ulisema ujumbe huo na kuongeza.

“Najuta kuuza nyumba ya Lumo ningejua nisingeuza. Asha peleka kabati la nguo kwa fundi panya wanakula nguo kila siku,” ulimaliza ujumbe huo.

Kwa mujibu wa Kamanda Komba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kueleza kuwa upelelezi bado unaendelea.

Katika tukio jingine mtu mmoja amekutwa dukani akiwa amefariki dunia katika eneo la kibene Kigamboni.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Mkoa wa Temeke, David Misime ambaye alimtaja marehemu kwa jina la Mbaraka Abdallah (28 ) mkazi wa Soweto ambaye alikutwa na mwajiri wake Ali Alfan mkazi wa Nunge.

Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa hauna jeraha lolote lakini uchunguzi umebaini katika uhai wake marehemu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kifua kikuu.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Vijibweni Kigamboni wilayani Temeke na kwamba upelelezi bado unaendelea.

Katika tukio jingine mwanamume mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Fikiri Urembo (35) mkazi wa Buguruni alikutwa amefariki dunia katika eneo la Osterbay baada ya kuangukia katika bwawa la kuogelea.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema mkasa huo ulitokea jana wakati marehemu akiwa kazini nyumbani kwa Omari Said (38) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Oysterbay.

Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela marehemu alikuwa akifanya kazi ya ulinzi hadi alipofikwa na mauti.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kwamba upelelezi wa tukio hilo bado unaendela.

Katika tukio jingine huko maeneo ya buguruni ulizuka moto katika jengo linalofahamika kwa jina la Dubai shopping center linalomilikiwa na Hamadi Hija(46) mkazi wa Temeke sokota.

Kamanda Komba alisema moto huo uliteketeza duka moja linalouza vifaa vya umeme, mali ya mpangaji Salumu Ali (39) mkazi wa Tandika Maputo.
Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment