na Shehe Semtawa
SHIRIKA la Kutetea Uhai wa Binadamu nchini (Pro-Life), limesema Tanzania haina haja ya kuingia katika kampeni ya uzazi za mpango kwa kuwa ni nchi yenye idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na mataifa mengine duniani.
Kauli hiyo ilitolewa na mtafiti wa elimu wa shirika hilo kutoka nchini Marekani, Brian Clowes, alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa mataifa makubwa yamelenga kupunguza idadi ya wananchi, ili yaendelee kupora rasilimali za Waafrika.
“Fedha za kampeni za uzazi wa mpango zimekuwa zikielekezwa kwenye nchi ambazo kwa kiasi kikubwa zina ongezeko la watu, hasa maeneo yenye watu weusi,” alisema Clowes.
Alisema hivi sasa nchi nyingi za Ulaya zimekumbwa na hofu ya kuwa na wazee wengi ukilinganisha na nchi za Afrika ambazo zinaonekana kuwa na vijana wengi.
Clowes alisema mwaka 1950, Ulaya ilikuwa na asilimia 22 ya watu ambapo Afrika ilikuwa na asilimia 9, hali inayoonesha kuwa bara hilo lilikuwa tupu.
Clowes alisema mwaka 1960, bara la Ulaya lilitangaza kampeni ya kudhibiti mimba ambapo hadi mwaka 1997, idadi ya watu imezidi kupungua na inakadiriwa ifikapo mwaka 2050, litakuwa na asilimia nane ya watu huku Afrika idadi yake ya watu ikiongezeka na kuwa asilimia 21.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment