Sunday, August 19, 2012

UKAHABA WA KUTISHA WAIBUKA KIGAMBONI DAR ES SALAAM


Florence Majani
YUMKINI, wengi wanaposikia neno hili Loliondo akili zinaweza kuhamia kwa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapila, maarufu kama Babu aliyepata umaarufu mwaka jana kwa kutibu maradhi mengi kwa dawa ya mitishamba iliyo katika kikombe.

 Lakini, Loliondo inayozungumziwa hapa si hiyo ya Babu wa Loliondo mkoani Arusha. Loliondo hii haina kikombe cha babu wala haitibu kwa mitishamba, bali ni eneo lililopo katika Kijiji Kichangani eneo la Kigamboni lenye upekee, likiwa umbali wa kilomita 40 kutoka katikati ya Jiji la Dar  es Salaam.

Upekee wake huo unatokana na majaliwa ya  ardhi yenye rutuba tele na uoto wa asili, lakini pia Kijiji cha Kichangani lilipo eneo la Loliondo lina mchanganyiko wa watu wa makabila zaidi ya matatu, asilimia 70 wakiwa ni Wasukuma.

Eneo hili lipo katika Kata ya Mbutu iliyopo Manispaa ya Temeke.

Baada ya kuvuka bahari kwa kutumia kivuko kutoka eneo la Kivukoni, yapo magari mengi  yanayoweza kukufikisha huko, ambayo wapigadebe wake hunadi maeneo maarufu wanayopita na utawasikia wapigadebe hao wakiita abiria " Mbutu- Kikwajuni – hadi Kichangani."

Ukishuka kituo cha mwisho wa gari, kinachoitwa Mbutu Kichangani, ukimuuliza hata mtoto mdogo Loliondo ni wapi hapa? Atakupeleka.

 Upekee mkubwa wa Loliondo ni kushamiri kwa biashara ya ukahaba, inayofanywa na wasichana wa  kuanzia umri wa miaka 13.

Loliondo ina nyumba zilizobatizwa jina la ‘ubanda’ na wenyeji wa eneo wakimaanisha vibanda. Nyumba hizo ndimo inapofanyika biashara hiyo pamoja na biashara ya kuuza pombe haramu ya gongo na bangi.

Wanawake wanaofanya biashara hiyo hapo Loliondo huitwa ‘wanawake wa ubanda’

Kwa nini eneo hilo likaitwa Loliondo?

Jina hilo linatokana na wanawake wanaotoa huduma ya ngono kuwaambia wanaume wanaotaka kupata huduma yao: “Ngoja nikapate kikombe cha Babu Loliondo."

Ndipo jina hilo lilizaliwa na kutumiwa zaidi ya wanaume hao, wakijaribu kutumia lugha ya kificho kwa safari ya kwenda huko, hata baadaye likakubalika na kuwa maarufu.

 Hamis Kashindye  ni mkazi wa Kichangani, Loliondo, kwa miaka 16 sasa, anasema kuwa kama ingepitishwa sensa kujua idadi ya wanawake wanaouza miili yao, basi wangeweza kuwa ni nusu ya wakazi wa eneo hilo.

 Anasema kuwa wanawake hao wanaofanya biashara ya ukahaba baadhi ni wakazi wa kudumu wa eneo hilo na wahamiaji kutoka maeneo ya Mbagala na Ilala.

“Hapa yapo mengi sana,(akimaanisha wanawake wanaojiuza) na kila siku yanaongezeka.  Wengine hawayapendi, lakini mimi naona yanasaidia sana,” anasema Kashindye  kwa lafudhi ya Kisukuma.

 Anaitetea kauli yake kwa kueleza kuwa wapo wanaume wasioweza kutongoza wanawake, hivyo wanarahisishiwa kazi kwa kutumia fedha zao kibindoni.

Anasema kuwa wanawake hao huwalenga wavuvi na wakulima wengine wa eneo hilo, ambao baada ya kupata fedha zao huzitumia kwa starehe.

 “Kama wavuvi na wakulima wa hapa wakishapata hela, wanamaliza hata Sh100,000 kwa hao wanawake wa ubanda,” anasema Kashindye akifafanua kuwa baadhi ya wanawake hao wana tabia ya kuhama hama wakifanya biashara hiyo na zaidi wakienda maeneo ya visiwani, Mafia na Bagamoyo.

Wanawake hao wanasemaje?

Juhudi za kukutana na wanawake hao zilifanyika kwa takribani wiki moja na haikuwa rahisi kukutana na kuzungumza nao.
Nilitafuta vijana wawili wenyeji wa eneo hilo, wanaofahamiana nao na kuongozana nao hadi Liliondo.
Baada ya kuwasili Loliondo, macho yangu yalilakiwa na nyumba ya udongo yenye uzio wa makuti, yenye vyumba viwili, upande mmoja ikiwa imebomoka na kuacha uwazi mkubwa.

Nje niliwakuta wanawake takriban 13, walikuwa wamekaa katika mabenchi, wengine wakishughulika kuuza pombe na sigara.

Wanaume watano walikuwa wakinywa pombe haramu ya gongo huku wakivuta sigara na bangi.

Pembeni anaonekana msichana mmoja, mweupe  aliye na umri usiozidi miaka 20 akinywa bia na kuvuta sigara, huku akiwa amekumbatiwa na mwanaume wa makamo, wakifanya mambo yasiyofaa kuelezewa gazetini.
Kushoto anaonekana binti mwingine akinywa pombe na kumnywesha gongo mwanaume wa makamo.
Wengine walikuwa wakiendelea na kazi ya kujaza pombe ya gongo katika chupa za konyagi na kuuza sigara kwa wateja wao.
Katika eneo hili kila mmoja yupo kwenye shughuli yake, hakuna anayemshangaa mwenzake.
 Vijana nilioongozana nao wanauliza kama watapata bangi, lakini mwanamke mmoja anawajibu kuwa bangi ilikuwepo, lakini imeibiwa.

Vitendo vinavyofanyika katika eneo hilo havionyeshi kama vinafanyika kijijini, unaweza kuhisi uko Uwanja wa Fisi au maeneo mengine jijini Dar es Salaam, vinapofanyika vitendo hivyo.
Nilitumia dakika 40 katika eneo hilo na kubaini kuwa mwanamke aliyekuwa na umri mkubwa kuliko wote Loliondo, ndiye kinara wa kundi, akijulikana kwa jina la Mama Nasra.
Baada ya kufuatilia nilibaini kuwa muda huo Mama Nasra alikuwa akisuka mipango ya kuwauza mabinti waliokuwepo kwa vijana waliofika Loliondo na kupokea fedha, huku akimtoa hofu mmoja wa wasichana hao kuwa mwanaume aliyemtafutia hana matatizo.
 “Wewe nenda kale sikukuu huko, kajipatie raha, unaogopa nini, mimi namfahamu huyo,”
alisikika Mama Nasra akisema.
 Wakati hayo yakiendelea mabinti wengine wanaoonekana ni wadogo zaidi, wanatoka ndani ya nyumba hiyo wakiwa wamejipamba.

Nilifanikiwa kuzungumza na Mama Nasra, ambaye ni kiongozi wa kundi hilo la wanawake wanaojiuza.
 
Katika mazungumzo yetu Mama Nasra anaeleza kuwa yeye na mabinti hao wapo hapo kwa ajili ya biashara nyingi ambazo ni kuuza gongo, bangi, sigara na ngono.

 “Wengine ni kipaji tu, au hulka. Hao watoto wengine walikuwa wanasoma. Wanapenda wenyewe kufanya kazi hiyo, mimi nawalea wasichana hawa na tunashirikiana katika biashara zetu,” anasema.

Anasema yeye siyo maskini na  anamiliki nyumba ya vyumba vitano na sebule maeneo ya Mbagala Rangi Tatu na anauza gongo kwa kuwa inalipa kuliko bia.

“Halafu sisi si wakazi hapa, siku mbili tatu tunahamia kambi nyingine, umeshanisoma?” anasema.

Wakati tukiendelea kuzungumza, binti mweupe akiwa amelewa anaelekea katika kichaka cha mahindi kilicho jirani akiwa na mwanaume waliyeketi naye awali.

Hata hivyo, Mama Nasra anawakataza wasichana hao kuzungumza chochote na kuwafukuza eneo hilo mara moja.
 “Si unawaona hao, wamepinda hao, usiwaone hivyo, wameshashindikana makwao,” anasema.

Kijana, mfanyabiashara wa  eneo hilo, Ally Shamte anasema kuwa biashara ya kuuza miili  Loliondo inafanyika kwa kiwango cha juu.

“Kuna mambo ya kutisha hapa. Yupo mama mmoja na mtoto wake wote wanafanya biashara hiyo, wanapika na pombe,” anasema.

“Wanawake hao wana mbinu mbalimbali za biashara yao, wapo wanaouza pombe za kienyeji, miguu ya kuku na vichwa vya kuku kama ushahidi, huku wakiuza miili yao kwa atakayehitaji huduma hiyo ambapo baadhi huishi kwenye nyumba kwa makundi.

Bei zao
Bei ya huduma ya ngono katika eneo hili zinatofuatiana kulingana na aina ya huduma anayohitaji mteja.

Shamte anasema kuwa kabla ya kuingia katika ngono mteja anaweza kuruhusiwa kushika maungo ya mwanamke kwa kuyakagua, pia mteja hupokelewa kwa baadhi wanawake kufunua nguo ili kukuvutia kabla kuelewana bei.

“Wanawake hao huwatoza wateja Sh1,000, kama atapenda kushika matiti, Sh1,500 hadi  Sh2,000 akishika sehemu za siri na kitendo kamili ni makubaliano yanayoanzia Sh 2,000,” anasimulia Shamte.

Matumizi ya Kondomu

Mbali ya kuuza miili yao siku zote wanawake hao husisitiza wateja wao kutumia kondomu na kwamba mtu anayekataa hunyimwa hudumu hiyo.

Ni kutokana na matumizi makubwa ya kondomu katika eneo hili la Loliondo ndiyo maana hivi sasa kuna malalamiko kwa baadhi ya wakazi wake kuwa mipira hiyo inatupwa ovyo mitaani na watoto kuitumia kupuliza hivyo kuhatarisha afya zao.

“Pale ukienda unawakuta na kondomu zao, ukikataa kutumia mpira hata uwe na fedha kiasi gani hawakupi. Ndiyo maana zinazagaa hadi watoto wanazigeuza maputo,” anasema Ally akiwasifu wanawake wa Loliondo.

Mwenyekiti wa Kijiji
 Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Paulo John alipoulizwa kama ana taarifa za  yanayofanyika katika eneo lake alidai hafahamu kama kuna biashara ya ukahaba.

“Nawajua wanawake hao, lakini walifika hapa kijijini wakisema kuwa wanataka kufanya biashara ya pombe ya kienyeji, mimi sifahamu kama wanajiuza,” anasema akiongeza:
 “Unajua hawa wanakijiji wanaogopa kunipa taarifa kwa kuhisi watachukiwa na wahusika au wataonekana wambea. Lakini kwa kuwa umenifahamisha, nitalifuatilia.”

 Wakati Mwenyekiti huyo akisema hafahamu yanayoendelea kijijini hapo, mgeni akifika na kuuliza nini kinfanyika Loliondo, hata watoto wadogo wanafahamu huku baadhi ya wakazi  wa kijiji hicho wakionyesha kukerwa na biashara hiyo na wengine wakitetea na kutaka iendelee kuwepo.

"Unajua bwana, hawa wanawake wamesaidia sana kupunguza mimba kwa wanafunzi na watu kuchukuliana wanawake," anasema Juma Saleh.

Anasema kuwapo kwa wanawake hao kumesaidia wanaotaka kupata huduma ya ngono kwa urahisi bila tatizo.
 Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment