Friday, August 24, 2012

WATOTO WA MITAANI KUONDOLEWA JIJINI DAR ES SALAAM

 
Elizabeth Edward
TAASISI ya Ustawi wa Jamii ikishirikiana na Shirika la Kimataifa linalojihusisha na watoto (Unicef), ipo katika mikakati ya kuwakusanya watoto wa mitaani waliopo jijini Dar es Salaam    na kuwaweka kwenye vituo kabla ya kuwarudisha katika mikoa waliyotoka.

Kamishna msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Rabikira Mushi alisema jana kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanya utafiti na kugundua idadi kubwa wa watoto hao waliopo jijini wametoka katika mikoa tofauti.

Alisema utafiti huo uliofanywa mapema mwaka huu umeonesha kuwa 81% ya watoto wanaorandaranda katika jiji la Dar es salaam wametoka katika mikoa mingine ambapo sababu kubwa iliyowaleta ni ugumu wa maisha katika maeneo wanayotoka.

“Tatizo hili ni kubwa kuliko tunavyodhani na ndiyo maana wenzetu wa Unicef wamekubali kutufadhili ili mradi kutekeleza mpango wa kutatua au kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani katika jiji la Dar es Salaam,” alisema Mushi.

Alisema kuwarudisha katika mikoa waliyotoka haitakuwa suluhisho ya tatizo hilo bila kubaini kilichowasukuma kuja mjini, kwa kutambua hilo ni lazima juhudi zifanyike kugundua mazingira waliyotokea na kujaribu kutatua kero zinazowakabili katika maeneo hayo.
Alisema kufanikisha hilo taasisi hiyo inashirikana na mashirika ya Makini, Kiwohede na Dogodogo Centre kuwakusanya watoto ambao watakuwa tayari kutoa taarifa za kweli kuhusu maeneo waliyotokea ili waweze kutengenezewa mazingira mazuri ya kurudi huko.

“Sio watoto wote wanaweza kukupa dondoo za kweli ila kwa wale ambao wataokuwa tayari kurudi katika mikoa wanayotoka tutawakusanya katika vituo hivi kuhakiki taarifa zao na kuwatengenezea mazingira mazuri ya huk wanakokwenda ili wasije kukumbana na changamoto zitakazowapelekea kurudi tena,” alisema Mushi.

Aliongeza kuwa jamii inapaswa kutambua tatizo hili linamhusu kila mmoja wetu na siyo kazi ya taasisi hiyo pekee hivyo inahitajika ushirikiano mkubwa kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira mazuri.

Kuhusiana na wazazi ambao huwatuma watoto wao kuomba omba katika mitaa alisema hilo ni kosa na wanaweza kushitakiwa kwa mujibu wa sheria ya watoto namba 21 ya mwaka 2009.
Kuhusu sense, Mushi alisema taasisi hiyo iko mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale wa mitaani, wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kuwa maeneo wanayozurura yanajulikana hivyo makarani wataelekezwa kupita huko kutekeleza majukumu yao.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment