Tuesday, September 18, 2012

Bwana harusi aliyekufa ghafla azikwa, majonzi yatawala msibani


Baadhi ya ndugu na jamaa wakibeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa bwanaharusi mtarajiwa marehemu Rashid Hamad, kabla yaq maziko jana. Marehemu  alikufa kwa ajali ya umeme masaa machache kabla ya kufunga ndoa huko Ukonga Mazambalauni, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. (Picha na Prona Mumwi)

Na Stella Aron

HATIMAYE aliyekuwa bwana harusi mtarajiwa Bw. Rashidi Omary aliyekufa ghafla saa chache kabla ya kufunga ndoa ya Kiislamu na Bi. Kuruthumu amezikwa jana.

Mazishi hayo yamefanyika katika makaburi ya familia yaliyopo Kimanzichana Mkuranga ambapo Bi. Kuruthumu alishindwa kuhudhuria mazishi baada ya kuzimia na kukimbizwa hospitali.


Umati mkubwa wa watu ulishiriki mazishi hayo wakiwemo madereva na makondakta wa daladala ambao walifahamiana na marehemu ambaye alikuwa akifanya kazi ya ukondakta.

Vilio na majonzi ndio yalitawala msiba huo ambao umevuta hisia za watu wengi ambao baadhi yao walizimia kutokana na mazingira ya kifo. 

Marehemu Omary alifaki ghafla juzi usiku wakati familia yake na ile ya Bi. Kuruthumu wakiwa kwenye mkesha wa ndoa iliyotarajiwa kufungwa juzi saa saba mchana.

Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo, baba mkubwa wa marehemu Bw. Ally Hatibu, alisema chanzo cha kifo hicho bado hakijafahamika kwani marehemu hakuwa akisumbuliwa na kitu chochote kabla ya kupatwa na umati.

"Leo (jana) saa 10 kasoro, tumemzika katika makaburi ya familia 
Kimanzichana na hakuna taarifa zozote kutoka kwa daktari na hatuna hisia za mtu kuhusika na kifo hiki,” alisema Bw. Hatibu.

Aliongeza kuwa, juzi usiku marehemu akiwa na rafiki zake, alikuwa akicheza rusha roho na baada ya muda aliamua kwenda kuoga kwani alikuwa amechaduka sana na baada ya kuingia ndani, muda mfupi alipiga kelele akisema “mama yala nakufa”.

Kutokana na mayowe hayo, walikimbia ndani na kumkuta akiwa chini na hali yake ilibadilika ghafla hivyo walimkimbiza katika Zahanati ya MICO iliyopo Mzambarani.

Madaktari walishauri akimbizwe katika Hospitali ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambako nao walishauri apelekwe Hospitali ya Amana kwa matibabu zaidi.

“Tulipofika Amana, wauguzi walimwingiza wodini na baada ya dakika chache, tulipewa taarifa kuwa bwana harusi amefariki dunia hivyo hata chanzo cha kifo chake familia hatuelewi,” alisema.

Alisema jana familia hiyo iliuchukua mwili wa marehemu hospitali, kuupeleka nyumbani kwao Mzambarauni Shule na kwenda kuzika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa maeolezo ya mwanafamilia mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema upo uwezekano wa marehemu kunaswa na umeme kwani eneo alilokuwa amesimama kulikuwa na soketi yenye shoti ya umeme na mwili wake ulikuwa na maji.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwa, Bi. Kuruthumu alikuwa na ujauzito wa marehemu.

Majira

No comments:

Post a Comment