POLISI Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya nchini, wamekamata dawa za kulevya za aina mbalimbali zenye uzito wa kilo 55,285 katika maeneo tofauti ya nchi tangu Januari hadi Desemba 15, mwaka huu.
Kukamatwa huko kumekwenda sambamba na kunaswa watu 6,929 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo ya mihadarati, huku idadi kubwa ikiwa ni wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 25 hadi 40.
“Hali hii inaonyesha wazi kuwa, wanawake wanashiriki kikamilifu katika kusafirisha dawa hizi,” alisema Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa na alisema na kuongeza:
“Sitaki kuzungumzia mtandao kama ni wa vigogo au watu wa kawaida, kikubwa ninachokifanya ni kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.”
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda Nzowa alisema dawa za kulevya aina ya cocaine zilikamatwa kilo 151, heroine (260), bangi 48,658 na mirungi kilo 6,216.
Zinavyoingizwa nchini
Kamanda Nzowa alisema baadhi ya dawa hizo zinaingizwa na Watanzania wenyewe kutoka nchi za nje na nyingine na raia wa kigeni kwa ajili ya kuziuza au kuzipeleka katika masoko mengine ya nje.
Alisema maeneo yanayotumika kusafirishia dawa hizo ni katika Bandari za Dar es Salaam na Tanga, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Pia alisema, wahusika wamekuwa wakitumia njia mbalimbali za panya kuingiza dawa hizo nchini.
“Tumefanikiwa kudhibiti maeneo mbalimbali ikiwamo viwanja vya ndege na bandari, lakini hawa jamaa ni wajanja na wamebadilisha njia za kuingiza dawa hizo nchini.
“Tunaendelea kupambana kwani baada ya kubana huku (bandari na viwanja vya ndege), tukabaini wanatumia bandari ndogo ya Bagamoyo, Mnazi Bay ya Mtwara kwa kuingiza au kusafirisha.”
Kamanda Nzowa alisema mpaka sasa kuna kesi 29 zilizopo Mahakama Kuu na watu 138 wanatuhumiwa kukutwa na cocaine, wakati 400 walikutwa na heroine. Alisema, kesi nyingine ziko katika Mahakama za kawaida ambako watu 5,544 wanatuhumiwa kukutwa na bangi na 847 mirungi.
“Tumejipanga kikamilifu kwa mwaka 2013 na zaidi ni kuhakikisha tunadhibiti maeneo yote yanayotumika kuingiza au kupitisha dawa hizo. Tumeweka mitego katika njia zote za panya na tukiwakamata wahusika tutawafikisha mahakamani,” alisema.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment