Thursday, February 21, 2013

KESI YA PONDA ISSA PONDA,MAHAKAMA YAPOKEA SILAHA KAMA KIELELEZO CHA USHAHIDI



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepokea silaha mbalimbali yakiwamo mapanga, visu, majembe, sufuria, makoleo na sufuria kama kilelezo katika kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49. 


Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne likiwamo la wizi wa mali yenye thamani ya Sh. milioni  59.6, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilika  isivyo halali.


Vielelezo hivyo vilitolewa na shahidi ambaye ni mpelelezi kutoka Mkoa wa Kipolisi Temeke, jijini Dar es Salaam, Thobias Walelo (34), mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa.



Mbali na silaha hizo, pia shahidi huyo aliwasilisha mahakamani hapo jenereta, mabegi mawili ya nguo, nyundo na ndoo za plastiki ambavyo vilipokelewa kama vielelezo vya  kesi hiyo.



Alidai kuwa Oktoba 12, mwaka jana, majira ya alasiri, alipokea jalada kutoka kwa bosi wake kwa ajili ya kulifanyia kazi.



“Nilipolisoma lilikuwa na taarifa kwamba kiwanja cha kampuni ya Agritanza Ltd kimevamiwa na Sheikh Ponda na wenzake,” alidai shahidi.



Shahidi huyo ambaye ni wa 10 wa upande wa mashitaka, alidai kuwa yeye alikuwa mhusika kupeleleza jalada hilo, akishirikiana na D/Ssgt Juma na D/Koplo Furaha, kwa kupitia maelezo ya mlalamikaji na nyaraka za mabadilishano ya ardhi hiyo kati ya kampuni ya Agritanza Ltd na Bakwata. 



Alidai kuwa yeye mwenyewe alikwenda Manispaa ya Temeke kwa Bwana Ardhi kufuatilia ukweli wa nyaraka hizo za mabadilishano ya ardhi na kupewa majibu kuwa eneo hilo linamilikiwa kihalali na kampuni ya Agritanza Ltd. 



Aliendelea kudai kuwa Oktoba 14, 2012, baada ya kupata picha hiyo kamili, akiwa na askari wenzake, walikwenda eneo la Chang’ombe Malkazi  na kukuta umati wa watu.



"Niliwaambia sikwenda kwa nia mbaya, nikawaomba waniteulie viongozi wao ili niongee nao,” alidai shahidi huyo. 



Aliongeza kudai kuwa waliwateua Sheikh Hussein Ismail, Sheikh Said Nyoni, Mukadam Swalehe na Mbaraka Daruwesh,  ili kupata uhalisia wa mawazo ya umati na nyaraka walizokuwanazo kuhusiana na eneo hilo. 

  

"Walipofika ofisini kwangu, niliwaomba nyaraka wakadai hawakuja nazo, niliwaomba niandike maelezo yao kuhusiana na kile wanachokilalamikia, wakataka yachukuliwe mbele ya wakili wao na wakaomba kwenda kumchukua. 



“Kwa kuzingatia kauli mbiu ya jeshi la Polisi  ya kutii sheria bila shuruti, niliwaamini waende wakamlete wakili wao ili mchana wa Oktoba 15, 2012, nichukue maelezo yao,” alidai shahidi huyo wa 10 wa upande wa Jamhuri. 



Alidai kuwa kabla ya kuwaruhusu alichukua namba zao za simu za mkononi baada ya kuwaruhusu,  hawakurudi tena.



"Nilipoona muda unakwenda, niliwapigia simu  wakaniambia: “Mheshimiwa, ukweli huko hatutarudi tena, tumia maelezo hayo hayo ya mdomo  tuliyokwambia sisi."



Baada ya kupata taarifa hiyo, niliandika barua kwenda Manispaa ya Wilaya ya Temeke na nikapata uthibitisho kuwa eneo hilo linamilikiwa na kampuni ya Chang’ombe Malkazi. 



“Niliwafahamisha wakuu wangu wa kazi, ikapangwa timu na Oktoba 16, 2012 kuamkia Oktoba 17, 2012, tulikwenda eneo hilo na kuwakuta watuhumiwa wote tukawakamata na kuwapelekea kituo cha polisi cha Kijitonyama kwa ajili ya mahojiano kasoro washtakiwa Mukadam na Ponda,” alidai shahidi huyo. 
 BY HELLEN MWANGO
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment