Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili nchini, Gilbert Buberwa amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa dengue.
Kifo cha Dk Buberwa kinafanya idadi ya watumishi
wa afya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo kufikia wawili baada
ya muuguzi Hamida Likoti kufariki dunia wiki iliyopita.
Ugonjwa huo uliolipuka mkoani Dar es Salaam,
umezua taharuki kwa wakazi wake kwa sababu hauna tiba na unasababishwa
na mbu, Aedes Egyptae, anayeuma mchana na anayeweza kuzaliana katika
majisafi yaliyotuama.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk
Primus Saidia alisema jana kuwa Dk Buberwa alifariki dunia saa saba
usiku wa kuamkia jana akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH).
Dk Buberwa alianza kuumwa ugonjwa huo akiwa kazini
katika Hospitali ya Temeke na kulazwa na hali yake ilipobadilika,
alihamishiwa MNH kwa matibabu zaidi.
“Kadiri siku zilivyozidi kwenda alibainika kwamba
viungo vyake muhimu, yaani ini na figo vimeharibika, hivyo alisafishwa
figo huku akiwa amelezwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
Dk Saidia alikumbusha kuwa virusi vya dengue
havina tiba isipokuwa dalili zake ambazo ni homa, kuumwa kichwa na
viungo vya mwili – ndizo zenye tiba.
Dk Buberwa alianza kuugua Mei 3, mwaka huu na siku
iliyofuata alipelekwa hospitali na mkewe ambako alilazwa ili kupata
uangalizi wa karibu wa madaktari wenzake.
Kaka wa marehemu, Wakili Nickson Ludovick alisema:
“Tunasubiri ndugu kutoka Bukoba na Musoma kwa mazishi yatakayofanyika
hapa Dar es Salaam katika makaburi ya Kinyerezi keshokutwa.”
Madaktari, wauguzi walazwa
Dk Malima alisema hadi jana, wafanyakazi tisa wa Hospitali ya Temeke walikuwa wamelazwa kutokana na homa hiyo.
Alisema wafanyakazi hao ni madaktari watano,
wauguzi watatu na mtaalamu mmoja wa maabara. “Kwa kipindi cha wiki mbili
zilizopita tumepokea wagonjwa wa dengue waliothibitika 15,” alieleza Dk
Malima.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Temeke, Shamim Kanju alisema
wafanyakazi wanaendelea kuambukizwa kutokana na kuwa katika mazingira
hatarishi kwa muda mrefu. Mtaalamu wa maabara, Eliud Kishebuka ambaye ni
mmoja wa wagonjwa waliothibitika kuwa na homa hiyo, alisema alianza
kujisikia mgonjwa juzi asubuhi, hivyo akaamua kwenda kufanya vipimo
Mwananyamala ambavyo vilithibitisha kuwa ameambukizwa.
Utambuzi wa ugonjwa
Dk Saidia alisema wataalamu wa vipimo hawajaelekezwa ipasavyo namna ya kutambua mgonjwa huo.
Alisema endapo mgonjwa atachukuliwa kipimo kamili
cha damu (full blood picture) na kuona kupungua kwa chembehai mgando
nyeupe za damu, wajue kwamba hicho ni kiashiria kikuu cha ugonjwa wa
dengue.
Mwandishi The Citizen augua
Mwandishi wa Gazeti la The Citizen, Mkinga Mkinga ni miongoni mwa watu walioambukizwa ugonjwa huo.
Mkinga alisema jana kwamba alianza kuhisi homa na
maumivu makali ya kichwa tangu Jumanne iliyopita na alipokwenda
hospitali ilibainika kuwa ni homa ya dengue.
“Nilipewa dawa za kutuliza pamoja na kunywa maji
mengi, kwa sasa niko nyumbani kwangu ninaendelea nazo lakini kichwa bado
kinauma na homa inakuwa kama ya vipindi,” alisema.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema wagonjwa wa dengue wameongezea na kufikia 399 hadi jana.
Ofisa mwandamizi wa wizara hiyo, Dk Janeth Bugamba
alisema jana kuwa kuna uwezekano wa idadi ya wagonjwa kuwa kubwa zaidi
kwa kuwa hakuwa amepata takwimu kutoka hospitali zote.
Msemaji wa MNH , Aminiel Aligaesha alisema wagonjwa wa dengue wanaongezeka kwa kasi katika hospitali hiyo.
Alisema hadi kufikia jana, wagonjwa 65 walifika
katika hospitali hiyo na kutibiwa kisha kurejea nyumbani na wengi ni
kutoka maeneo ya jirani na hospitali hiyo wakiwamo wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Muhimbili (Muhas) ambao hata hivyo, hakutaja idadi yao.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment