Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Sasa ni dhahiri kwamba kuna msuguano wa wazi kati ya mihimili
miwili ya dola, Bunge na Serikali, kuhusiana na hatua ya Serikali
kuchelewa kutekeleza maazimio ya Bunge.
Msuguano huo umeshika kasi wiki hii baada ya
Serikali kuwarudisha kwenye nyadhifa zao vigogo wawili wa Wizara ya
Maliasili na Utalii ambao hivi karibuni waliondolewa na Waziri Lazaro
Nyalandu, huku wabunge wakiapa kuibana Serikali kuwang’oa viongozi hao.
Vigogo hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori,
Profesa Alexander Songorwa na Mkurugenzi Msaidizi, Jaffar Kidegesho kwa
madai ya kutowajibika ipasavyo katika vita dhidi ya ujangili nchini.
Mbali na sababu hiyo, lakini Nyalandu alikaririwa
akisema alichukua uamuzi huo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mazimio
16 ya Bunge, yaliyotolewa baada ya taarifa ya Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Ikulu yatoa tamko
Wakati mvutano huo ukiendelea, Ikulu imeitaka wizara hiyo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kumfukuza mtu kazi.
Katibu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema
kuzingatiwa sheria, kanuni na taratibu za kumfukuza mtu kazi ndiyo
suluhisho la msuguano unaoendelea kati ya Waziri Nyalandu na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi juu ya hatima ya
wakurugenzi hao ambao walitimuliwa kazi Februari mwaka huu.
Balozi Ombeni aliwataka viongozi hao kuhakikisha
kuwa uamuzi wowote wanaoufanya kuhusu kuwaondoa kazini watumishi hao
unazingatia sheria, taratibu na kanuni kwa kuwa zinaeleza wazi hatua
zinazopaswa kuchukuliwa.
“Siwezi kujua kwa nini wanaendelea kuvutana, hilo
waulize wao, ninachojua wanatakiwa wazingatie sheria, kanuni na taratibu
katika jambo hilo,” alisema.
Alipoulizwa ni nani kati ya Nyalandu na Tarishi
hafuati sheria za utumishi wa umma, alisema: “We mwenyewe nenda kazisome
(sheria) utajua tu.”
Kwa mujibu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka
2002, Kifungu cha IV (23) (2) inayozungumzia mamlaka ya Rais kumwondoa
mtumishi aliyemteua kazini, amri ya kumfukuza mtumishi wa umma
itatekelezwa iwapo
(a)hati ya mashtaka imeandikwa dhidi yake
(b)mtumishi wa umma amepewa nafasi ya kujibu mashtaka hayo
(c)Maombi yametolewa kwenye hati ya mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizo chini ya kifungu namba 34.
Ripoti ya uchunguzi wa matatizo katika utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza Ujangili, azimio namba saba lilimhusu Profesa
Songorwa kwa jina lake na cheo chake likitaka Serikali kumwajibisha kwa
kuudanganya umma kuhusu mazingira na kifo cha Emiliana Marrow wa Babati.
Uchunguzi wa madaktari huru na picha za mwili wa
marehemu, zilionyesha alikufa kwa kuteswa na askari waliotekeleza
Operesheni Tokomeza Ujangili, lakini taarifa ya Profesa Songorwa ikasema
alikufa kwa Pressure (shinikizo).
“Bunge linaazimia Serikali ichukue hatua za
kumwajibisha mkurugenzi wa wanyamapori kwa kuudanganya umma na kujaribu
kuficha ukweli,” linasomeka azimio hilo la Bunge la Desemba 20.
Hata hivyo, baada ya Nyalandu kumwajibisha Profesa
Songorwa na mwenzake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maimuna Tarishi
aliwarejesha kazini akidai kukiukwa kwa sheria za utumishi wa umma.
Wabunge mbalimbali waliohojiwa jana, walidai
kinachoonekana kinatoa taswira kwamba Serikali inalitunishia misuli
Bunge kila mara linapotoa maazimio ya kuwawajibisha watumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Wabunge hao, siyo mara ya kwanza
hali inayotokea sasa ndani ya Wizara ya Maliasili kutokea serikalini,
kwani mazingira kama hayo yalitokea pia Wizara ya Nishati na Madini.
Mwaka 2011, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, David
Jairo alirudishwa kazini baada ya kusimamishwa kazi kutokana na
kutuhumiwa bungeni kuchangisha zaidi ya Sh50 milioni ili zisaidie
kupitisha bajeti.
“Yanayotokea sasa Maliasili ni kama yaleyale
yaliyotokea Nishati na Madini… Inaonekana kama ni sinema vile,
tunapitisha (Bunge) maazimio lakini Serikali haitaki kuyatekeleza,”
alidai mbunge mmoja.
Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), David Silinde alisema kinachotokea Wizara ya Maliasili na
Utalii ni mwendelezo wa Serikali kupuuza maazimio ya Bunge.
“Hata kwenye Hazina tulitaka TPDC (Shirika la
Maendeleo ya Petroli) libakie na asilimia 100 ya makusanyo lakini mpaka
sasa Serikali imepuuza na inalipa asilimia 50 tu,”alidai Silinde.
Silinde aliongeza kusema, “ Hii ni tabia inayoanza kujengeka na
sisi kama wabunge hatupaswi kuiacha izoeleke kwa hiyo mimi ni mmojawapo
ambaye nitalihoji hili Bunge la bajeti wiki ijayo.”
Kwa mujibu wa Silinde, mpango wake huo unaungwa
mkono na wabunge wengine na kwamba watataka maazimio yote
yaliyokwishaazimiwa na Bunge yawekewe kikomo cha utekelezaji.
Mbunge wa Bunda, Alphaxard Kangi Lugola ambaye
alikuwa mwiba kwa Serikali na kuchangia mawaziri wanne kujiuzulu,
alisema ameshtushwa na taarifa za kurudishwa kazini kwa vigogo hao.
“Mimi ndiyo kwanza niko uwanja wa ndege narejea
sijasikia kama wamerejeshwa, lakini kama ni kweli basi kuna tatizo ila
subiri nithibitishe hili ili nikisema niseme nikiwa na uhakika,”alisema
Lugola.
Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya, alisema
kilichofanywa na Serikali kuwarudisha vigogo hao kimejenga mazingira
mabaya ya utendaji kazi kati ya Nyalandu, Tarishi na vigogo hao.
“Huku ni kumdhalilisha Nyalandu kwa sababu hata
kama angekuja waziri mwingine yeyote ni lazima atekeleze maazimio hayo
ya Bunge… kama kuna kasoro wazirekebishe lakini wawajibishwe,”alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema maazimio hayo hayakuwa
yake kama Lembeli wala ya kamati bali yalikuwa ni ya Bunge zima.
“Hayo yanayotokea huko Maliasili nisingependa
kuyazungumzia ila ninachoweza kusema maazimio ya kuwawajibisha watendaji
hao yalikuwa ni ya Bunge zima na bado yanasimama kama yalivyo,”alisema.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment