TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali
imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Balozi wa Malawi
hapa nchini Hayati Mhe. Flossie Gomile Chidyaonga kilichotokea juzi
Ijumaa tarehe 09 Mei, 2014. Balozi Chidyaonga alifariki akiwa njiani
kupelekwa hospitali ya Aga Khan ya hapa Dar es Salaam.
Balozi
Flossie Chidyaonga alizaliwa tarehe 16 Juni, 1960 huko Blantyre nchini
Malawi. Balozi Chidyaonga aliitumikia Serikali ya Malawi katika nyadhifa
mbalimbali. Kati ya mwaka 2006 hadi 2010 alikuwa Naibu Balozi wa
Malawi nchini Uingereza na baadaye Kaimu Balozi hadi alipoteuliwa kuwa
Balozi wa Malawi hapa Tanzanaia.
Siku
ya Jumatatu, tarehe 05 Mei, 2014, Balozi Flossie Chidyaonga alishinda
vizuri na kufanya shughuli zake kama kawaida. Hata hivyo, ilipofika
usiku, alijisikia vibaya na kupelekwa hospitali ya Aga Khan, Dar es
Salaam ambapo alipatiwa Matibabu na kuwekwa mapunziko kuanzia saa 6
usiku hadi saa 12 asubuhi aliporuhusiwa na kupewa dawa za kutumia
nyumbani. Balozi Chidyaonga aliendelea kutumia dawa hizo na hali
kuonekana kuimarika hadi siku hiyo ya ijumaa, tarehe 09 Mei, 2014. Siku
hiyo, aliamka vizuri hadi ilipofika majira ya saa 6 mchana, hali yake
ilipobadilika na kukimbizwa tena hospitali ya Aga Khan ambapo
alipokelewa Daktari alisema amekwishafariki. Sasa hivi, Mwili wa
Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Uchunguzi
wa madaktari umeonesha kuwa marehemu amefariki kutokana na Mshipa Mkuu
wa AORTA kuvimba na kupasuka kulikosababisha damu kukusanyika kwenye
mfuko wa moyo na hivyo kufanya moyo ushindwe kufanya kazi yake.
Kesho
tarehe 12 Mei, 2014 mwili wa Marehemu utachukuliwa kutoka Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili na kupelekwa kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano
wa Julius Nyerere ambapo kutafanyika misa ya kumuombea Marehemu na kutoa
heshima za mwisho kuanzia saa 4 asubuhi. Mwili wa Marehemu unatarajiwa
kusafirishwa kwenda Blantyre, Malawi siku ya Jumanne tarehe 13 Mei, 2014
na mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 14 Mei 2014
huko Blantyer, Malawi.
Katika
kipindi chote alichokuwa mwakilishi wa Malawi hapa nchini, Balozi
Chidyaonga alifanya kazi yake ya kukuza na kuendeleza ushirikiano kati
ya nchi zetu mbili kwa umahiri wa hali ya juu. Siku zote alikuwa mstari
wa mbele kutoa ushirikiano kwa Serikali na Mabalozi wenzake
wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.
Mungu aiweke roho ya marehemu Balozi Flossie Chidyaonga, mahali pema peponi.
AMEN
Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Dar Es Salaam, Tarehe 11 Mei, 2014
No comments:
Post a Comment