Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ugonjwa wa homa ya dengue ambao umezidi kusambaa mkoani Dar es
Salaam na kuathiri wilaya zake tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni umezua
hofu na taharuki kubwa kwa wananchi. Takwimu za Kitengo cha Utafiti wa
Magonjwa cha Ifakara (IHI), kimeweka kambi katika Hospitali ya
Mwananyamala hapa jijini kutafiti aina za homa zinaonyesha kuwa, kwa
miezi miwili ya Machi na Aprili pekee, wagonjwa 85 walibainika kuwa na
ugonjwa huo.
Kwa siku tatu mfululizo kuanzia juzi, gazeti hili
limekuwa likichapisha habari za kusambaa kwa ugonjwa huo, ambao
madaktari mabingwa wa ugonjwa huo wamesema hali ni mbaya kuliko
inavyodhaniwa kwa kuwa asilimia 50 ya watu wanaopimwa na kubainika kuwa
na ugonjwa huo ni watu wazima kuanzia miaka 18.
Katika kuthibitisha kwamba ugonjwa huo haubagui au
kuweka matabaka, madaktari watatu na muuguzi mmoja wameripotiwa kuugua
ugonjwa huo, kama ilivyo kwa mmoja wa wanamuziki maarufu hapa nchini
ambaye hadi juzi alikuwa amelazwa katika hospitali moja hapa jijini
baada ya kuugua ugonjwa huo. Tunaambiwa kwamba hivi sasa kuna hali ya
hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo na kwamba sasa mbu ni hatari kuliko
ilivyokuwa awali, kwani hawa wanaoambukiza homa ya dengue ambayo haina
chanjo wala tiba wanaambukiza wakati wa mchana.
Hatuoni ajabu hali hiyo inapoleta hofu na taharuki
kwa wananchi, hasa pale mamlaka husika zinapothibitisha kwamba hapa
jijini kuna wagonjwa wapya 20 kila siku na kwamba asilimia 2.5 ya
wagonjwa huwa katika hali mbaya. Moja ya mambo yanayozidisha hofu ni
kwamba mgonjwa anapobainika kuambukizwa dengue hana tiba rasmi,
isipokuwa kinachotibiwa ni dalili tu. Taarifa kwamba kuna uhaba mkubwa
wa vifaa na vitendanishi pia hazileti matumaini kwa wananchi, ingawa
mamlaka hizo zimesema kuna wataalamu wa kutosha wanaoweza kubaini
ugonjwa huo.
Kinachotatanisha zaidi ni dalili za ugonjwa huo
ambazo siyo tofauti na zile za malaria. Je, kuumwa kichwa na kusikia
uchovu na maumivu ya viungo siyo dalili zilezile kama za malaria? Je,
ugonjwa huo kujitokeza kati ya siku tatu na 14 baada ya kuambukizwa siyo
dalili za ugonjwa huo? Tofauti kati ya ugonjwa huo na malaria ni kwamba
mgonjwa wa dengue hutoka damu sehemu mbalimbali za mwili kutokana na
kuharibika kwa chembehai nyeupe za damu. Vinginevyo magonjwa hayo ni
kama pacha wanaofanana na ndiyo sababu tunasema zinahitajika taarifa za
kutosha ili wananchi wajue la kufanya pindi wanapougua magonjwa hayo.
Sisi tunadhani Serikali inastahili lawama kwa
kutochukua hatua stahiki mapema kupambana na ugonjwa huo, ambao uliingia
Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kuua wanafunzi kadhaa wa
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Juni mwaka jana, Wizara ya Afya
ilithibitisha kuwapo kwa ugonjwa huo na Machi 26 mwaka huu, ilitoa
taarifa kwa umma, ikisema wagonjwa 70 walikuwa wamebainika, 58 kati yao
wakiwa Kinondoni, saba Temeke na watano Ilala.
Hata hivyo, wizara hiyo haikupaswa kuishia katika
kutoa taarifa tu pasipo kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi nchi
nzima kuhusu ugonjwa huo, namna ya kujikinga na nini cha kufanya iwapo
wataambukizwa. Ulihitajika uwazi badala ya usiri, vinginevyo ugonjwa huo
usingeenea kwa kasi tunayoishuhudia hivi sasa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment