Na Mwandishi Wetu
Serikali ya Tanzania
imeendelea kuweka misingi imara ya kufanyiakazi maoni ya wananchi kuhusu hali
ya utawala bora nchini kama yalivyobainishwa kupitia Ripoti ya Hali ya Utawala
Bora iliyoandaliwa na Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Itakumbukwa kuwa,
Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 kati ya 54 za AU zilizokwishajiunga na Mpango
wa APRM. Tanzania ilijiunga na mchakato huu mwaka 2004 na Bunge kuridhia mnamo
tarehe 1 Februari 2005.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Mei 11, 2014 na APRM Tawi la
Tanzania, imeeleza kuwa tayari Wizara mbalimbali zilizoguswa na Ripoti hiyo
zimekwishakuelekezwa kufanyiakazi changamoto zilizobainishwa na kutoa taarifa.
“Baada ya Rais Jakaya
Kikwete kuiwasilkisha Ripoti ya Tanzania mbele ya Wakuu Wenza wa Nchi za APRM
mwaka jana, Serikali ilitakiwa kuanza kufanyiakazi changamoto za kiutawala bora
zilizobainishwa.
“Utekelezaji huo
unaendelea vyema. Masuala mengi ya kikatiba yameingizwa kwenye rasimu
inayojadiliwa. Masuala ya kisera na kitaasisi tayari yamefikishwa katika
taasisi husika kwa ajili ya kufanyiwakazi,” ilisema taarifa hiyo.
APRM ni nyenzo mojawapo
ya kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa shughuli za maendeleo na
ujenzi wa utawala bora kote Barani Afrika ikiwemo Tanzania katika ili
kutafakari kwa pamoja namna bora Zaidi ya kuziendeleza juhudi hizo.
“Mpango huu wa
kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi
wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa
Afrika na unatoa fursa kwa wananchi kutathmini hali ya utawala bora katika nchi
zao na kuendeleza dhamira ya serikali ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala
bora nchini kwa kuwashirikisha Wananchi wake,” imesisitiza sehemu ya taarifa
hiyo.
Ripoti ya APRM Tanzania
ambayo itatumika kama rejea muhimu, imeeleza kwa kina juhudi za Tanzania katika
kulinda amani. kuimarisha utawala bora na wa sheria na jitihada katika kulinda
haki za binadamu.
Hata hivyo Ripoti hiyo
pia imegusia changamoto zinazopaswa kufanyiwakazi ambazo ni suala la kushughulikia
kero za Muungano, kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo,
kuimarisha zaidi juhudi za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya nchi na ujenzi
wa utawala bora.
Kuhusu mchakato wa sasa
wa Katiba unaendelea taarifa hiyo imesisitiza: “Tumeaswa kuutumia vyema
mchakato wa sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika
miaka mingine mingi ijayo.”
No comments:
Post a Comment