Monday, July 7, 2014

ILALA SASA KUFUNGA VIWANDA VINAVYO TIRIRISHA MAJI MACHAFU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa
Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam  ipo mbioni kufunga viwanda vinavyotiririsha maji machafu kwenye makazi ya watu wilayani humo.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam  na Angelina Malembeka, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na  Huduma za Jamii manispaa hiyo.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza  kwa niaba ya Meya wa Ilala, Jerry Slaa, (pichani) kwenye mkutano mkuu wa wa Y2K Social Klabu iliyoanzishwa kwa lengo la kushughulikia kero zinazo ikabili jamii ya kata ya Kiwalani.

Angelina alisema kumekuwapo na malalamiko mengi yanayofika manispaa, lakini wanapotoa onyo kwa wamiliki wa viwanda yamekuwa hayatekelezwi na wahusika.

Angelina alisema baadhi ya viwanda pamoja na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kuwa ni moja ya maeneo yanayotiririsha maji machafu kwa wananchi kwa kipindi kirefu sasa.

“Sasa kitakachofuata ni kufungia viwanda na maeneo yote sugu yanayochafuwa mazingira kwa makusudi na kuhatarisha maisha ya wananchi,” alisema Angelina.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Y2K Social Klabu, Fatma Mwasora, alisema toka kuanzishwa kwa klabu hiyo wamekuwa wakipambana na changamoto za kuweka mazingira ya Wilaya ya Ilala katika hali ya usafi  na kwamba kwa kiwango kikubwa lengo hilo limefanikiwa.

“Changamoto ni nyingi hasa kwenye  vituo vya  afya kumekuwa na rushwa ambazo zinawakatisha tamaa wananchi kuamini huduma zinazotolewa na watendaji wa Serikali,” alisema Fatma.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment