Tuesday, May 19, 2015

WAANDISHI WAASWA KUPIGA VITA RUSHWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAANDISHI wa Habari wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wametakiwa kutumia kalamu zao kupambana na rushwa sambamba na kusisitiza demokrasia na utawala bora katika nchi zao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliwaasa waandishi wa habari walioshiriki katika mkutano wa saba wa wadau wa habari na wafanyabiashara wa Afrika Mashariki (EAC-EABC) alipokuwa akifunga mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
“Vyombo vya habari ni njia ya kupambana na rushwa, kama vitaamua kupambana kikamilifu itaweza kufanikiwa,” alisema Membe.
Membe alisema waandishi wa habari wakikaa kimya na kutozungumzia rushwa pamoja na kuhamasisha utawala bora watakuwa hawatendei haki nchi zao pamoja na EAC.
Awali akisoma maazimio ya mkutano huo kwa Waziri Membe ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema mkutano umekubaliana kuboresha hali ya ufanyaji kazi kwa mwandishi wa habari sanjari na kuangalia ulinzi wa maisha yake.
Aidha mkutano huo umependekeza nchi wanachama kutangaza na kuunga mkono tuzo za waandishi wa habari zinazotolewa na EAC-EABC kwenye vyomba vya habari kuhakikisha zinapatikana kazi bora za waandishi wa habari kwa ajili ya kushindanishwa.
Katika hafla hiyo pia waandishi 23 kutoka nchi wanachama wa EAC walipokea tuzo mbalimbali pamoja na kuzawadiwa fedha katika tuzo za EAC-EABC.
Chanzo:Habari Leo

No comments:

Post a Comment