Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na. Benedict Liwenga-Maelezo.
JESHI
la Polisi limewataka wananchi kuwa makini ili kuepukana kutapeliwa
fedha na watu wasio waaminifu wanaojipatia fedha hizo kwa njia ya simu
na mitandao.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Mrakibu
Mwandamizi (SSP), Advera Bulimba wakati akiongea na Mwandishi wa Idara
ya Habari kwa njia ya simu ambapo amesema kuwa jamii hainabudi
kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwaibua watu wanaojihusisha na
uhalifu kwa njia ya laini za simu pamoja na njia ya mtandao kwa kutoa
taarifa mapema katika vituo vya Polisi.
Ameongeza
kuwa, watu wanatakiwa kuwa makini kabla ya kutuma pesa kwa watu
wanaodaiwa kuhitaji kutumiwa pesa ili kujiridhisha nao na kuepuka
kutapeliwa.
‘’Jeshi
la Polisi limekuwa likifanyia kazi taarifa zinazotolewa na walalamikaji
kwa kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani ambapo mpaka hivi
sasa tayari kuna baadhi tumewafikisha mahakamani na baadhi wanatumikia
vifungo vyao,’’alisema Bulimba.
Aidha,
pamoja na juhudi za Jeshi la Polisi katika kjutoa elimu kwa umma
kuhusiana na wizi wa mtandao, amevitaka vyombo vya Habari pamoja na
wadau wengine kutoa elimu hiyo pia kwa jamii kuhusiana na wizi wa aina
hiyo.
‘’Zoezi
hili la kuwabaini wahalifu kwa njia ya mtandao ni endelevu ili
kupunguza ama kuondoa kabisa uhalifu wa aina hii’’, alisisitiza Bulimba.
Kwa
upande wake Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) Bw. Innocent Mungy amesema kuwa wizi kwa njia ya simu na mitandao
ni makosa ya kiuhalifu ambayo yanapaswa kuripotiwa Polisi ili hatua
stahiki ziweze kuchukuliwa.
Amesisitiza
kuwa watu wasithubutu kutuma fedha kwa watu bila kujiridhisha kwani
kuna baadhi ya watu hutumia vitambulisho bandia katika kusajili laini
zao za simu na hivyo hutumia kufanyia uhalifu kwa kutuma ujumbe mfupi wa
maneno kwa watu kwa lengo la kuomba pesa.
‘’Sisi
kama TCRA tunatoa elimu kwa umma ili wananchi waepuke kutapeliwa na pia
tunawashauri kuripoti mara moja matukio ya uhalifu kwa njia za simu na
mitandao katika vituo vya Polisi kwa uchunguzi na hatua stahiki,’’
alisema Mungy.
Hivi
karibuni matukio ya wizi kwa njia ya simu na mitandao yamekuwa
yakijitokeza ambapo baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakituma
ujumbe mfupi wa maneno na kuomba pesa kwa ndugu na jamaa ili kujipatia
fedha kwa njia ya utapeli.
No comments:
Post a Comment