SERIKALI
YALIFUNGA GAZETI LA MSETO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua
kulifungia kwa miezi 36 gazeti la “MSETO”. Amri ya kulifungia Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali
Na. 242 lililotolewa tarehe 10 Agosti, 2016. Uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa
Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 Sura ya 229, kifungu 25(1).
Kifungu hicho kinasema “Waziri akiona kwamba kwa ajili ya manufaa ya umma au kwa ajili ya
kudumisha amani na usalama inafaa afanye hivyo aweza kutoa amri na kuitangaza
kwenye Gazeti la Serikali ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri
hiyo litakoma kutolewa tangu siku (ambayo katika fungu hili itaitwa ''tarehe ya
kuanza kutumika'') itakayotajwa katika amri hiyo”
Uamuzi huo unazuia gazeti la Mseto kuchapishwa katika
njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao (Online publication) kwa
mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
Aidha, hatua hii ya kulifungia gazeti hilo
imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu
kuanzia Septemba, 2012 hadi Agosti,
2016 kumtaka Mhariri wa gazeti kuacha
kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizo zingatia maadili
ya taaluma ya uandishi wa habari bila mafanikio.
Kutokana na hali hiyo, Serikali kwa masikitiko
makubwa, imelazimika kuchukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa
gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo na kughushi kwa kutumia nyaraka
mbalimbali za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wa Serikali kwa lengo kutaka kumchonganisha na wananchi ambao wamekuwa na
matarajio makubwa kwa uongozi wa Awamu ya Tano.
Pamoja na
makosa mengine, hivi karibuni gazeti lao katika toleo Na. 480 la tarehe 4 hadi
10 Agosti, 2016 lilichapisha na kusambaza makala na barua ya kugushi kutoka Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO) yenye kichwa cha habari kisemacho “Waziri
Amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano.
Kwa mujibu wa vyombo vya uchunguzi vya Serikali,
imebainika kwamba nyaraka hiyo imeghushiwa na wahariri na walipotakiwa kuleta
uthibitisho wa nyaraka waliotumia katika gazeti lao, walishindwa kuleta
vithibitisho huo.
Ninatoa wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na
watangazaji wa habari kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya
uandishi wa habari ambayo ukizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha
Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia
maadili, weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana
navyo
Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya
Kimataifa inayoanisha uhuru na mipaka ya habari kama vile Tamko la Kimataifa la
haki za Binadamu la mwaka 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na
Kisiasa, na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu 1981.
Mikataba na matamko hayo kwa pamoja licha ya kuanisha
uhuru wa habari ambao Tanzania imeruhusu kwa kiwango kikubwa pia, imeweka ukomo
wa uhuru huo kwa kukataza habari za uongo, uzushi na uchochezi.
Ninapenda kusisitiza
kwamba Serikali itaendelea kujenga uhusiano mzuri na wa kirafiki kati yake na
wadau wa sekta ya habari. Aidha ninasisitiza tena wadau wa sekta hii kuzingatia
Sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kujenga heshima
ya tasnia ya habari na kulinda amani ya nchi yetu.
Mhe. Nape M. Nnauye (Mb,)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
No comments:
Post a Comment