Mshiriki
Mkuu wa Shindano la Kanumba Star Search, Florence Mutegoa (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya AM Arts
Promotion pamoja na Mdhamini wa Shindano la “Kanumba Star Search” kwenye
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya
Habari (MAELEZO) leo tarehe 03.08.2016 Jijini Dar es Salaam,
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mshiriki Mkuu wa Shindano la
Kanumba Star Search, Florence Mutegoa (Mama Kanumba) amezindua shindano
la kusaka vipaji vya waigizaji watakaoigiza filamu itakayoenzi maisha ya
Marehemu Steven Kanumba.
Uzinduzi huo umefanywa leo Jijini
Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambapo
Mshiriki Mkuu wa Shindano hilo ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa
wingi kudhamini shindano hilo litakaloibua vipaji vipya vya uigizaji.
“Tunatambua thamani ya maigizo
ndio sababu tumeamua kuanzisha shindano hili ili kuibua vipaji
vilivyojificha, hivyo tunawakaribisha wananchi wote wenye uwezo wa
kuigiza waje washiriki kwenye mashindano yetu pia tunaomba wadhamini
kujitokeza zaidi ili watusaidie kufanikisha shindano hili”, alisema
Mutegoa.
Mutegoa amefafanua kuwa shindano
hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Kanumba the Great Film
na Kampuni ya AM Arts Promotion ambapo hadi sasa shindano hilo lina
mdhamini mmoja kutoka Kampuni ya simu za mkononi za KZG – Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya AM Arts Promotion, James Mwombeki amesema kuwa
marehemu Kanumba alikuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza nchi
kimataifa pamoja na kuibua vipaji vya wasanii wa maigizo hivyo hatuna
budi kumuenzi kwa kuiendeleza Sanaa ya uigizaji.
“Sisi kama AM Arts Promotion
tumeamua kushirikiana kwa pamoja na Mama Kanumba kufanya shindano hili
kwa nia ya kuendeleza tasnia ya filamu nchini kama vile marehemu Kanumba
alivyokua akijitahidi kuwapa fursa ya uigizaji watu wa kila rika”,
alisema Mwombeki.
Naye, Msanii wa filamu, Mayasa
Mrisho amewasisitiza wananchi kushiriki kwa wingi kwenye mashindano hayo
kwani Sanaa ya uigizaji ni njia mojawapo ya kujipatia kipato na kuinua
maisha ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Mkurugenzi wa Kampuni ya
Simu za Mkononi za KZG – Tanzania, Raymond Kalikawe amesema kuwa
wamekubali kuwa wadhamini wa shindano hilo kwa kuwa ukuzaji wa vipaji
vya wasanii wa maigizo ni jambo muhimu pia amewaomba wadhamini wengine
kujitokeza zaidi kusaidia shindano hilo.
Shindano hilo linatarajiwa kuanza
mwezi Septemba mwaka huu, litaanzia Mikoa ya Kanda ya ziwa na baadae
kuendelea katika Mikoa mingine.Washindi wataigiza filamu ya kumuenzi
marehemu Kanumba itakayojulikana kama “Maisha ya Kanumba.
No comments:
Post a Comment