Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mkurugenzi
wa Idara ya habari (MAELEZO) Bw. Hassan Abbas amesema kuwa ujio wa
msanii wa maigizo kutoka nchini Marekani Bi. Toussaint Duchess maarufu
kama Mama Lucy uwe changamoto kwa wadau wa sanaa nchini.
Akizungumza
kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa
Nape Nnauye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa igizo la msanii
Lucy linaloitwa Mama Lucy anakwenda Afrika (Mrs. Lucy goes to Africa)
mwishoni mwa wiki Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi
Abbas alisema kuwa ni vyema wadau wa sanaa wakatumia ujio huo kama
changamoto itakayowasaidia kujifunza na kuwa wabunifu zaidi katika kazi
zao za sanaa.
“Ujio
wa muigizaji Lucy ni changamoto kwa wadau wa sanaa nchini, ni fursa ya
kujifunza kwa wasanii hususani katika eneo la sanaa za jukwaani, vile
vile ni fursa kwa vijana wa kitanzania ambao wanatarajia kufanya kazi
za sanaa” alisisitiza Bw. Abbas
Aliendelea
kwa kusema kuwa Serikali inatoa pongezi kwa kituo cha televisheni cha
Azam na wasanii mbalimbali wakiwemo Suzan Lewis (Natasha) na Yvone
Cherry (Monalisa) ambao wameshiriki kwa ubunifu wa kumleta msanii huyo
nchini pamoja na maboresho mengine yanayofanywa na kituo hicho cha
televisheni cha Azam.
Aidha,
aliongeza kuwa akiwa Msemaji wa Serikali, anatarajia kushirikiana na
wadau wa sanaa nchini kupitia mikakati mbalimbali itakayoandaliwa ili
kuunga mkono juhudi aliyoanza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli
katika kujali na kusimamia kazi za sanaa na wasanii ili waweze kunufaika
na kazi zao.
Kituo
cha televisheni cha Azam kinatarajiwa kuonesha igizo hilo la msanii
huyo kutoka nchini Marekani liloandaliwa kwa kushirikiana na wasanii
mbalimbali kutoka nchini wakiwemo Suzan Lewis (Natasha) na Yvone Cherry (Monalisa) pamoja na filamu mbalimbali zitakazofanywa na msanii huyo.
No comments:
Post a Comment