Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
10/08/2016
Dar es Salaam
Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametoa wito kwa viongozi
wa dini nchini kupitia mahubiri na dua kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya
kupambana na ujangili nchini.
Wito
huo umetolewa leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha
“Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kilichoandaliwa na Kamati ya
Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es salaam.
Waziri Maghembe amesema kuwa Viongozi wa dini wakiongeza neno juu ya ujangili wa wanyama hao itasaidia roho za waumini kujua umuhimu wa wanyama hao na kuwatendea mema kwani nao wana haki ya kuishi kama viumbe wengine.
“Katika
ibada zetu za jumapili na ijumaa tujitahidi kutoa mahubiri na dua kwa
jamii ili kufikisha ujumbe juu ya kuwalinda wanyama hawa na kupambana na
ujangili ndani ya nchi yetu”, amesema Waziri huyo.
Aidha
amesema kuwa idadi ya tembo mwaka 1990 hadi 1994 walikuwa takribani
laki tatu na nusu(350,000), mwaka 2009 walikuwa 45,000 na mwaka jana
idadi ya tembo hao walikuwa 55,000 hivyo jamii kwa ujumla imetakiwa
kuwalinda wanyama hao.
Mbali na hayo Waziri Maghembe alizitaja faida za wanyama kuwa ni
pamoja na kuongeza pato la taifa kwa asilimia 15.5 na kuweza kutoa
ajira takribani Watanzania milioni moja katika Sekta ya Utalii na
kusaidia katika mzunguko wa uotaji wa baadhi ya mbegu.
Kwa
upande wake Mwandishi wa Kitabu hicho Mchungaji Christosiler Kalata
amesema kuwa lengo la kuandaa kitabu hicho ni kuwaelemisha na kuitaka
jamii kutunza uumbaji wa Mwenyezi Mungu wakiwemo wanyama.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WILDAID Peter
Knights ambao ni wadhamini wa kitabu hicho, ameipongeza Serikali ya
China kwa jitihada zake za kupiga marufuku biashara ya uuzaji wa meno ya
Tembo hatua hiyo imesaidia kulinda wanyama hao.
No comments:
Post a Comment