Wednesday, August 10, 2016

Waziri awataka Maafisa Mawasiliano Serikali kufanyakazi kimkakati


Frank Mvungi-Maelezo
Maafisa Mawasiliano Serikalini wametakiwa kufanya kazi zao kimkakati ili kuongeza ufanisi  katika utendaji wao hasa kwenye kipindi hiki cha Awamu ya Tano.

Akizungumza  leo Jijini Dar es salaam na Wakuu wa  Vitengo vya Mawasiliano Serikalini wa Wizara na Taasisi za Serikali Waziri wa zamani wa Habari wa Jamhuri ya watu wa China, Mhe. Zhao Qizheng amesema ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa mawasiliano yote yanalenga kuwainua wananchi wake.

“Msemaji wa Serikali inabidi uwe makini katika kazi zako kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati”, alisema Qizheng.
Akifafanua Mhe. Qizheng amesema kuwa ili Tanzania Iweze kufikia maendeleo ya kweli ni muhimu kujenga mfumo dhabiti wa Mawasiliano ya Serikali kwa Umma.

Katika kutekeleza majukumu yao Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kama wasemaji ni lazima wawe na uelewa mpana kuhusu masuala yanayohusu sekta wanazosimamia ili kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wananchi.
Pia aliwataka Wasemaji wa Serikikali kujiandaa kabla ya kujibu hoja mbalimbali za kitaifa na Kimataifa zinazohusu Serikali na wananchi ili kutoa taarifa sahihi  kwa Vyombo vya haabari.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Hassan Abbas amesema ni dhamira ya Serikali kuwasiliana kimkakati ili kuchochea maendeleo.

“Lengo letu ni Kuhakikisha kuwa tunafanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa mawasiliano ya Serikali na wananchi ili kuwapa fursa ya kutoa mrejesho”alisema Abbas.

Katika kuhakikisha azma hiyo inatumia Abbas amebainisha kuwa kwa sasa Serikali inajipanga kufanya maboresho ya mifumo ya Mawasiliano ya Serikali.

Aidha Mawasiliano ya Serikali katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya Tano yanalenga kubadilisha maisha ya wananchi kutoka hali duni kwenda kwenye hali bora.

Mkutano kati ya Waziri wa Zamani wa Habari wa China na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini wa Wizara na Taasisis za Serikali umelenga kujenga uwezo wa Wasemaji wa Serikali ili waweze kuwasiliana na Wananchi kimkakati.

No comments:

Post a Comment