*Asema mazingira mazuri ya uwekezaji chini ya uongozi wa
Mhe. Rais Dkt. Samia yamechochea mafanikio
Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),
Bw. Masha Mshomba amefichua siri ya mafanikio makubwa ambayo NSSF imeyapata
kuwa yamechangiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyohamasisha wawekezaji katika sekta
binafsi, kuweka mazingira mazuri na kuwezesha kupata waajiri na wanachama wengi
wapya katika sekta binafsi.
Bw. Mshomba amesema hayo tarehe 3 Julai, 2024 wakati alipotembelea banda la
NSSF mara baada ya ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar
es Salaam (DITF) maarufu SabaSaba yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Tanzania
Sehemu Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji." Maonesho hayo yamefunguliwa
na Mhe. Filipe Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji akisindikizwa na mwenyeji
wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda hilo la NSSF, Bw. Mshomba
amesema kwa mujibu wa taarifa za hesabu ambazo hazijakaguliwa katika mwaka wa
fedha 2023/2024, thamani ya NSSF kwa sasa inafikia trilioni 8.5 sawa na
ongezeko la asilimia 77% ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita.
“Ongezeko hili ni kubwa hasa ukizingatia kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita
ukuaji wa NSSF umekuwa mkubwa mno, hivyo tunampongeza sana Mhe. Rais Dkt.
Samia kwa juhudi anazoweka katika kuhakikisha mazingira ya biashara hapa nchini
yanakuwa mazuri ambayo yamechangia mafanikio haya,” amesema Bw. Mshomba.
Amesema wakati NSSF inaendelea kutekeleza mpango wake wa maendeleo unaoishia
Juni 30, 2026, wanatarajia thamani ya Mfuko kufikia trilioni 11 ambayo itakuwa
ni zaidi ya mara mbili ukilinganisha na kipindi ambacho Rais Dkt. Samia
alipoingia madarakani.
Bw. Mshomba amesema kwa sasa NSSF imeelekeza nguvu ya kuwafikia wanachama wapya
waliopo katika sekta isiyo rasmi ili waweze kujiunga na kuchangia katika NSSF
kwani tayari wameshaweka mifumo mizuri ya usajili na uchangiaji pamoja na mafao
yanayovutia kupitia Mpango wa Kitaifa wa Sekta Isiyo Rasmi.
Amesema ushiriki wa NSSF katika maonesho hayo ni kwa ajili ya kutoa elimu ya
hifadhi ya jamii kwa wanachama na wadau kuhusu huduma mbalimbali ambazo NSSF
unazitoa zikiwemo usajili wanachama kutoka sekta binafsi na sekra isiyo rasmi,
uchangiaji, kulipa mafao, uwekezaji pamoja na uhakiki wa wastaafu.
Bw. Mshomba amesema pia wanatumia maonesho hayo kuwaeleza wanachama mambo
makubwa ambayo NSSF imeyafanya kupitia huduma za TEHAMA ambapo sasa wanachama
wanaweza kujisajili kupitia lango la huduma binafsi kwa mwanachama (Member
Portal) na lango binafsi kwa mwajiri (Employer Portal).
Amesema NSSF inaendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini hivyo
wataendelea kuboresha huduma zao mbalimbali.
No comments:
Post a Comment