KAMATI YA BUNGE, USTAWI NA MAENDELEO YA JAMII YAWATAKA WATUMIAJI DARAJA LA NYERERE, KIGAMBONI KULIPIA BANDO


*Yasema matumizi ya bando ni nafuu na yanaondoa usumbufu

*Yaipongeza NSSF kwa kuweka mifumo katika Daraja hilo

Na MWANDISHI WETU,

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imeridhishwa na utaratibu wa manunuzi ya bando la tozo kwa matumizi ya Daraja la Nyerere, Kigamboni ambapo imewataka watumiaji wa daraja hilo kulipia bando kwa sababu ni nafuu, rahisi na linapunguza msongamano na kuongeza mapato.

Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo, Novemba 11 2024, ilipotembelea miradi ya NSSF ukiwemo wa Daraja la Nyerere, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatma Toufiq, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na NSSF katika Daraja hilo hususan ya kuweka matumizi ya bando.

“Tunaendelea kuipongeza Serikali na wenzetu wa NSSF kwa kazi nzuri sana ambayo imefanyika pale Daraja la Nyerere kiukweli kumewekwa mifumo mizuri ambayo licha ya kupunguza changamoto ya foleni lakini pia inapunguza mianya ya upotevu wa mapato,” amesema Mhe. Fatma.

Amesema Kamati pia inamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoleta maendeleo nchini kwa manufaa ya wananchi na kuwa wanaunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita na kuwa wanaamini Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ukiwemo wa NSSF utaendelea kuleta tija kwa wanachama kupitia uwekezaji unaofanywa na Mifuko hiyo.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mhe. Katani Katani amepongeza mfumo wa manunuzi ya bando katika Daraja hilo na kuwataka wananchi kujiunga kwani ni mfumo rahisi na rafiki na pia unaondoa foleni.

Naye, Mhe. Mariam Kisangi amesema mradi wa Daraja la Nyerere umechochea maendeleo ya wananchi wa Kigamboni, ambapo amewataka kuendelea kulipia tozo za kupita kwa kutumia bando kwani inapunguza usumbufu.

Kwa upande wake, Mhe. Athumani Maige amewataka wananchi kuendelea kutumia matumizi ya bando wakati wanapopita katika Daraja hilo na pia ameipongeza NSSF kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesisitiza elimu iendelee kutolewa kwa wananchi na watumiaji wa Daraja kutumia malipo ya bando kwani ni rahisi na inapunguza usumbufu.

“Matumizi ya bando ni mazuri na yataongeza mapato, kupunguza kero kwa watumiaji wa Daraja hivyo ni muhimu wananchi kupewa elimu zaidi ili watumie bando kuondoa usumbufu,” amesema. 

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema wanaendelea kuwahamasisha watumiaji wa Daraja kulipia bando la siku, wiki au mwezi ili waweze kupita kwa urahisi hasa ukizingatia kuwa matumizi ya bando ni nafuu zaidi.

Bw. Mshomba ameipongeza kamati hiyo na kuahidi kuwa maoni, maelekezo na ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo wataufanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji.




KANISA LA AICT WAUNGA MKONO AGENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

DAR ES SALAAM - AICT

Kanisa la Uaskofu la AICT Pastorate ya Magomeni  Dayosisi ya Pwani lililopo Jijini Dar es Salaam limetoa msaada wa Mitungi ya Gesi 20 kwa akina mama wanaoishi maeneo jirani na Kanisa hilo ikiwa sehemu ya shamrashamshara kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa hilo.

Msaada huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania AICT  Musa Massanja Mwangwesela ambaye pia ni Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Mwanza ambapo amesema kuwa kutolewa kwa msaada huo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania juu ya utunzaji wa Mazingira kupitia Nishati Safi ya kupikia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa shina Namba 3 Makubusho Suleimani ally Mohamed amelishukuru Kanisa hilo pamoja na Viongozi wa Kanisa hilo kwa wema wao wa kutoa msaada wa Nishati hiyo ya kupikia katika Mtaa wa Uwarani na Maswa.

Nao baadhi ya Wanufaika wa Msaada huo akiwemo  Judith Kobelo na Mariamu Gumbo wameshukuru kwa kupewa msaada huku wakisema Nishati hiyo itakavyokwenda kurahisisha upatikanaji wa Nishati hiyo safi ambayo wamekabidhiwa.

Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la Uaskofu la AICT Pastorate ya Magomeni  Dayosisi ya Pwani lililopo Jijini Dar es salaam ni Tarehe 27/10/2024, Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania






















NSSF YAKUTANA NA WAHARIRI NCHINI


*Yatambulisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Sekta Isiyo Rasmi (NISS)

 

*Sasa mwanachama kufungua madai ya mafao kidijitali ‘online’


*Yaweka kipaumbele cha matumizi ya TEHAMA, zaidi ya asilimia 82% sasa zinafanyika kutumia mifumo


* Yatoa Tuzo kwa Vyombo vya Habari vinavyotekeleza vyema sheria ya NSSF, yatambua mchango wa wahariri wastaafu


Na MWANDISHI WETU,

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba ameanika mafanikio mbalimbali ambayo Mfuko umeyafanya yenye lengo la kumuondolea kero mwanachama na kumsogezea huduma huko huko aliko kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Pia ametambulisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS).


Bw. Mshomba ameeleza mafanikio hayo tarehe 1 Oktoba 2024 wakati akifungua mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioshirikisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Nchini, uliofanyika katika ukumbi wa NSSF Mafao House Ilala, Dar es Salaam.


Amesema wanaipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya NSSF hasa katika miaka minne iliyopita ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na wanachama katika Mfuko tofauti na kipindi cha nyuma na kupelekea thamani ya Mfuko kufikia trilioni 8.5 tofauti na trilioni 4.8 wakati alipokuwa anaingia madarakani. 


Bw. Mshomba amesema NSSF inaendelea kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA na sasa shughuli nyingi za NSSF zinafanyika kupitia mifumo na kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25, huduma zote muhimu zitatolewa kupitia mifumo, aidha alifafanua ya kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za Mfuko zinafanyika katika Mifumo tofauti na asilimia 42 ya mwaka 2021/22


“Kupitia mifumo ya TEHAMA, NSSF imeweza kuwafikia kwa ukaribu wanachama na wadau wake ambapo kwa sasa hawalazimika kufuata huduma ofisini badala yake wanazipata huko huko waliko na hivyo tumewaondolea adha ya kufuata huduma umbali mrefu,” amesema Bw. Mshomba.


Aidha, amesema NSSF imezindua mfumo unaomuwezesha mwanachama kufungua madai ya mafao kwa njia ya mtandao na kuwa lengo ni kumrahisishia mwanachama kupata huduma karibu zaidi bila ya kufika katika ofisi za NSSF. Pia Mfumo huu utaondoa kabisa usumbufu kama ulikuwepo na pia utawawezesha wanachama wetu tunaowahudumia kupata huduma kwa wakati, kwa kuwa mifumo hii ni wazi na ufuatiliaji unakuwa rahisi.


Kuhusu sekta isiyo rasmi, Bw. Mshomba amesema Mfuko umechukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wengi wanahamasika kujiunga na kujiwekea akiba, ambapo kwa sasa unaendelea kutoa elimu kupitia makundi mbalimbali na kuwaeleza faida za kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na ya baadaye.


Aidha, kuanza kwa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS), ni utekelezaji wa mipango mahsusi iliyowekwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) (Millenium Goals) ambayo pamoja na mambo mengine inataka watu wote kuwa kwenye hifadhi ya jamii. Mshomba alifafanua kuwa NSSF imeshaweka mikakati ya kutosha kuwafikia watu wote ikiwa ni kwa makundi na hata mwananchi mmoja mmoja. Wananchi wote watakaojiunga na NSSF watapata Mafao na Huduma mbalimbali kama ambavyo wafanyakazi wengine wote wanapata.

Uwepo wa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS) utatoa fursa ya kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma hizi ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa nchi, utasaidia juhudi za Serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi, utaongeza nguvu za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa Nchi na mwisho utachochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Bw. Mshomba amesema pia NSSF ina Skimu ya uchangiaji wa Hiari ambayo inawahusu watumishi wote. “Natumia nafasi hii kuhamasisha na kuwataka mchangie kupitia skimu hii kwa sababu kufanya hivyo mtajikuta mnapata kipato cha ziada, kazi kubwa mbele yetu ni kutoa elimu ili watu wengi wapate uelewa wa jambo hili.” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa  Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amepongeza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na NSSF hasa katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo wa kukamilisha kiwanda cha sukari Mkulazi. Pia amepongeza NSSF kuweka mipango sasa ya kuwafikia wananchi wote walioko katika Sekta isiyo rasmi kwani kwa kufanya hivyo sasa watu wote tutakuwa ni wamoja na hapo baadaye wote tutanufaika, safari ya uzee ni ya kila mmoja wetu na hivyo ni vizuri kila mmoja akifika awe na uhakika wa kesho yake.

Balile alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waajiri wa sekta binafsi hasa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao NSSF kwa wakati ili wanapostaafu waweze kulipa stahiki zao. 

“Leo tumepata bahati tumepata ushuhuda kutoka kwa wastaafu waliokuwa wafanyakazi kutoka katika vyombo vya habari ambao ni wanufaika wa mafao ya kustaafu na pensheni ya kila mwezi Bi. Flora Wingia na Bw. Bakari Machumu” Aidha, wahariri wastaafu wamepewa Tuzo kwa kutambua mchango wao.

Akiwasilisha taarifa ya uendeshaji wa Mfuko, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Omary Mziya amesema NSSF inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.

Bw. Mziya amesema wanaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa hifadhi ya jamii ili kuongeza uelewa wa haki ya kujiunga kwenye Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi  (NISS) na kuendelea kuboresha mifumo na kusogeza huduma karibu na jamii.

“Sekta isiyo rasmi ina Watanzania takribani 11 Millioni, hawa wote wanahitaji kinga dhidi ya majanga ambayo ni uzee na majanga mengine yanayoweza kutokea hapa kati, kuachishwa kazi ama kufariki na kadhalika”. 

Sekta isiyo rasmi inatoa nafasi kwa Watanzania wote kujiunga na hifadhi ya jamii, Mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, biashara ndogo ndogo, mama lishe/ Baba lishe, bodaboda na wasafirishaji wengine, machinga, wanahabari wa kujitegemea.































 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa