na Shehe Semtawa
MKAZI wa Kariakoo Mtaa Agrey jijini Dar es Salaam, Ahamad Selemani anashikiliwa na Polisi baada mita yake ya Luku kukutwa na uniti za umeme 29,365.5, zenye thamani ya sh milioni nane.
Meneja wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Kanda ya Ilala, Athanasius Nangali, alisema jana kuwa mteja huyo ambaye jina analotumia kwenye mita yake ya Luku ni Mallick Bhachool, hajawahi kununua umeme tangu alipounganishiwa mita hiyo mwaka 2010.
Mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Kwa mujibu wa Nangali, tukio lingine kama hilo limetokea katika eneo la Kariakoo Mtaa wa Magila ambapo Meneja wa Hoteli ya Akubu Paradise, Inocent Masawe alikamatwa akiwa na uniti 1100 za umeme kwenye mita yake ya Luku, zenye thamani ya sh milioni 4.
Alisema mteja huyo amekuwa akifanya ujanja wa kununua umeme kidogo kwa ajili ya matumuzi ya hoteli yake, lakini umeme uliomo kwenye mita ni mwingi kuliko kiasi anachonunulia.
“Hawa tutakula nao sahani moja hadi watuambie wanakonunua umeme na hatimaye tutakamata mtambo unaozalisha uniti hizo bandia,” alisema.
Nangali alisema TANESCO itahakikisha inawatia mbaroni wauzaji wa uniti hizo kinyume cha sheria.
“Hawa kuna sehemu wananunua umeme lakini hatujafahamu ni wapi hivyo kukamatwa kwao ni dalili kubwa ya kubaini wanakonunua maana katika hali ya kawaida haiwezekani mtu awe na uniti hizi zote,” alifafanua Nangali.
Alitoa wito kwa Watanzania kutoa taarifa za wanaoihujumu TANESCO na kutangaza zawadi ya sh 50,000 kwa kila nyumba itakayokamatwa.
Alipoulizwa kuhusu ongezeko la faini na idadi ya watu waliofikishwa mahakamani, Nangali alisema idadi hiyo itajulikana mara baada ya kufanya majumuisho mwishoni mwa mwezi huu japo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 100 sasa wameshakamatwa na kulipishwa faini tangu kuanza kwa operesheni hiyo.
Wiki tatu zilizopita aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, William Mhando, alitangaza kukamatwa kwa watu watatu mkoani Dodoma na wawili jijini Dar es Salaam waliokuwa wakitumia umeme ambao haujafahamika unakopatikana.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment