Home » » Madiwani K’ndoni wasusia uchaguzi wa Naibu Meya

Madiwani K’ndoni wasusia uchaguzi wa Naibu Meya


Na Evans Magege, Dar es Salaam
MADIWANI wa vyama viwili vya upinzani (Chadema na CUF) wa Manispaa ya Kinondoni wamesusia kikao maalumu cha uchaguzi wa Naibu Meya.

Wakizungumza Dar es Salaam juzi, madiwani hao walisema walichukua uamuzi huo baada ya kugundua kikao hicho kiliitishwa kinyume cha Sheria na Kanuni zinazotumiwa na baraza hilo.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Baraza hilo, Boniface Jackob, alisema wameshangazwa na uongozi wa baraza hilo kuwaandikia barua za dharula za kutaka kufanya kikao maalumu ambapo walipofika ukumbini wakakuta ajenda ya kikao hicho ni kufanya uchaguzi wa Naibu Meya.

Alisema walipohoji ni kwanini uchaguzi huo unafanywa katika kikao maalumu na si mkutano mkuu, hapakupatikana majibu.

“Kuanzia sasa tumeamua kutangaza mgogoro rasmi na uongozi wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Kinondoni kwa sababu wameamua kuitisha uchaguzi batili wa kumchagua Naibu Meya.

“Tulisambaziwa barua kwamba tuhudhurie kikao maalumu, hatukujua kuna kitu gani kitakachojadiliwa lakini tuliyoyakuta ni madudu tupu.

“Kwanza tumefika tukakuta taratibu zimebadilika kwa kusainishwa posho za kikao kabla ya kikao kuanza na baadaye tunatajiwa ajenda kuu ni kufanya uchaguzi wa Naibu Meya, jambo hilo lilitushangaza na kutulazimu tususie kikao hicho ambacho kinaonekana kukumbatia mazingira ya ufisadi .

“Tukauliza mbona wanafanya uchaguzi huo kwa njia ya kulazimisha, wakabaki na kigugumizi huku madiwani wa CCM wakishinikiza ni lazima uchaguzi ufanyike, sisi tukasema hatuna tatizo na uchaguzi lakini uchaguzi huo si utavunja kamati zote na kusukwa upya, kwa maana hiyo miradi iliyokuwa ikisimamiwa na kamati hizo si itakosa muendelezo wa usimamizi mzuri lakini hawakutuelewa.

“Tukaendelea kuwadadisi kwa vipengele vya kanuni kuwa hadi sasa bado hatujafanya mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka ambao ungetuwezesha kupata taarifa za utendaji na uwajibikaji wa halmashauri na kisha uchaguzi wakabaki wanatoa macho, basi nasi tumeamua kususia mkutano huo kwa sababu ni uchaguzi batili,” alisema Jackob.

Hata hivyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, alisema uchaguzi huo ni halali na umefuata taratibu zote.

Alisema ameshangazwa kitendo hicho cha madiwani wa upinzani kugoma na kutoka nje ya ukumbi lakini akasema jambo hilo halikuharibu utaratibu mzima wa kupiga kura ambapo walibaki wajumbe 30 waliopiga na kumuwezesha Songolo Mnyonge kuibuka mshindi kwa kura zote za wajumbe.

“Uamuzi wao haujazuia uchaguzi wetu na kama wamesusia mbona hawakuzisusia posho walizozichukua asubuhi,” alihoji Mwenda.

Chanzo: Mtanzania







0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa