na Nasra Abdallah
ZOEZI la kumpatia kila mwananchi kitambulisho cha uraia huenda lisifanikiwe kutokana na utaratibu ambao umekuwa ukitumika katika ujazaji fomu kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa taarifa gani hasa wanazotakiwa kuwa nazo katika ujazaji wa fomu.
Baadhi ya waandikishaji wamekuwa wakiwataka watu kuleta vyeti vya kuzaliwa, kitambulisho cha kupiga kura, leseni ya gari na kitambulisho cha kazi, wakati sehemu nyingine wakiambiwa ni kitambulisho kimojawapo tu kinachotakiwa.
Upungufu mwingine ni idadi ndogo ya makarani pamoja na kasi ndogo ambapo huchukua takriban dakika 20 hadi 25 kumhudumia mtu mmoja.
“Ili uweze kuwahi hapa inakupasa uje sio zaidi ya saa 4:00 asubuhi kwani ukichelewa itabidi uandikishwe tu kesho,” alisikika karani mmoja katika kata ya Mikocheni.
Hata hivyo, baadhi ya makarani walisema wanalazimika kujaza wenyewe fomu kwa kuwauliza wananchi maswali, kwa vile wengi wao wamekuwa wakijaza kwa makosa na hivyo kuchafua au kuharibu fomu.
Aidha, wananchi wengi hususan vijana hawajui majina yote ya wazazi wao wala kata walizozaliwa au namba zao za simu kitendo kinachowafanya kuanza kupiga simu kwa wazazi wao au ndugu zao kuuliza huku karani akiwa anasubiria majibu hayo.
Imebainika kuwa hakuna usiri wowote wakati wa uandikishaji huo kwa kuwa wakati mtu aliye nyuma ya anayeandikisha husikia kila kitu.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umegundua kwamba wageni wengine hawataki kujulikana.
Katika namna ya kushangaza, baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakitumia mwanya huo kuhamasisha wanachama wake kujiandikisha kwa wingi kama njia mojawapo ya kuwa na wapiga kura wengi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Khamis Juma, alisema walitegemea utaalamu zaidi utumike kupunguza kupotea kwa muda mwingi wa wananchi ambao wangekuwa katika shughuli za uzalishaji mali.
Naye Amina Salum alisema alitegemea siku ambayo waandikishaji walienda kuandikisha majina nyumbani wangejaza na fomu ili kuepusha usumbufu ambapo unapaswa kwenda kwa mara nyingine tena katika ofisi ya mtendaji.
“Lingine linalotushangaza ni kwamba unatakiwa kuleta picha yako,” alihoji dada huyo.
Wananchi wengi waliiomba Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) kutoa elimu zaidi ya nini hasa wananchi wanatakiwa kujaza katika fomu hizo ili wakifika kwa makarani iwe rahisi na kuepusha misongamano isiyo ya lazima.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Dickson Maimu alisema elimu ya uandikishaji imetolewa kwa kiasi kikubwa, na kwamba ni hali ya kutozingatia maelekezo hayo.
Alisema kuwa kuhusiana na wingi wa nyaraka, ni jambo jema kwa mtu kuwa na vitambulisho vingi, ingawa sio vibaya kuwa na kitambulisho kimojawapo.
“Hata pale ambapo kwa bahati mbaya hana kiambatanisho chochote, atakuwa na barua ya afisa mtendaji wa mtaa inayomtambulisha na ataandikishwa,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vema kuwa na uhakika wa taarifa za watu kwa sababu vitasaidia kumjulisha kuwa yeye ni Mtanzania kwa kujua amesoma wapi, shule gani, umri wake na mambo kama hayo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment