Home » » MAITI YAOKOTWA UFUKWENI DAR

MAITI YAOKOTWA UFUKWENI DAR


na Efracia Massawe
WATU watano wamefariki dunia katika matukio tofauti jijini Dar es Salaam juzi, likiwemo la mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30 kukutwa amekufa kandokando ya Bahari ya Hindi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela akizungumza na waandishi ofisini kwake jana, alisema mwili wa mwanaume huyo ulikutwa majira ya saa 3 asubuhi eneo la Ununio, huku ukiwa hauna jeraha.
Marehemu ambaye amehifadhiwa hospitali ya Mwananyamala alikutwa amevaa suruali nyeusi na shati la drafti.
Kamanda Kenyela alilitaja tukio jingine kwamba huko barabara ya Kawawa Road eneo la Mikumi, Magomeni majira ya saa 8:45 usiku gari isiyofahamika ikitokea Kigogo kwenda Mikumi ilimgonga mtembea kwa miguu ambaye hakufahamika jina lake ila anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30-35 na kumsababishia kifo chake.
Kwa mujibu wa Kenyela, mwili wa marehemu ambaye alikuwa amevaa bukta ya rangi ya damu ya mzee bila shati, umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alisema majira ya saa 9 alasiri huko Kigamboni Mji Mwema eneo la Family Beach, Daud Masima (30) mkazi wa Kitunda akiwa na wenzake wakiogelea alizama na mwili wake haujapatikana hadi sasa.
Aidha, alisema tukio jingine lilitokea makutano ya Barabara ya Ohio Garden saa 11.45 jioni ambako gari namba T 187 ADT Toyota Corolla ikiendeshwa na dereva asiyefahamika, lilimgonga mwendesha pikipiki Bakari Mcholombe (23) mkazi wa Mtongani kwa Azizi Ally na kumsababishia kifo.
Misime alisema Mcholombe alikuwa akiendesha pikipiki namba T 906 BRR SanLG huku akiwa amembeba abiria mwanamke anayekadiriwa kuwa na miaka 45-50, aliyepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mwili wa marehemu ameifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na majeruhi anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa