na Betty Kangonga
ZIKIWA zimesalia siku mbili kabla ya kufanyika kwa zoezi la sensa ya watu na makazi, mzozo wa posho umeibuka katika kituo cha Makumbusho kati ya makarani na watumishi wa Idara ya Taifa ya Takwimu.
Hali hiyo imetokea baada ya waratibu hao wa sensa kutaka kuwalipa fedha pungufu makarani hao tofauti na makubaliano, huku makarani hao wakitishia kuharibu madodoso watakayopewa katika kazi ya sensa.
Mzozo huo ulianza majira ya saa 3:00 asubuhi katika kituo cha Makumbusho baada ya waratibu wa sensa kutaka makarani hao walipwe fedha za siku nne badala ya saba.
Wakizungumza na gazeti hili jana, makarani hao walisema kitendo kinachofanywa na serikali, sio cha kiungwana kwani chaweza kusababisha kasoro kwenye kazi ya sensa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Andrea Lameck, alisema wameshiriki semina kwa siku saba, lakini viongozi wa serikali Wilaya ya Kinondoni na waratibu wa sensa, walitaka kuwalipa fedha za siku nne.
“Tangu wiki iliyopita tunahangaishwa malipo yetu. Leo tumekuja kufuatilia matokeo yake tunaambiwa tulipwe sh 140,000 badala ya sh 245,000. Hatukubali hadi tulipwe hela zetu zote,” alisema.
Naye Rose Munisi, alisema kuna uwezekano mkubwa wa serikali kushindwa kupata tathmini halisi ya sensa kutokana na ubabaishaji unaofanywa na waratibu wa zoezi hilo.
Mmoja wa waratibu wa sensa, Japhet Maiga alifika katika eneo hilo na kuwataka makarani hao kuwa na subira ili manispaa iweze kutafuta fedha za kuwalipa.
Maiga aliyekuwa katika gari namba SM 2861, alishindwa kuafikiana na makarani hao na kuamua kuondoka.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Amon Herman, alisema kata yake ina zaidi ya vijana 246 wanaopaswa kulipwa.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment