Home » » MTIKILA KUFUNGWA JELA LEO?

MTIKILA KUFUNGWA JELA LEO?



Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, anatarajia kuhukumiwa leo mahakamani. Mtikila atahukumiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam, kutokana na kesi inayomkabili ya kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete, kwamba anataka kuuangamiza Ukristo.

Hukumu hiyo itatolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkuu Mkazi, Illivin Mugeta anayeisikiliza.

Mchungaji Mtikila alifunga ushahidi baada ya kutetewa na mashahidi wawili badala ya kumi alioahidi kuwafikisha mahakamani hapo.

“Mheshimiwa, nafunga ushahidi, ilikuwa nilete mashahidi 10, lakini wawili wanatosha kwa sababu wengine walikuwa maaskofu kutoka Mwanza ambao naamini wangekuja kueleza kile kile nilichoeleza.

“Nahofia kupoteza fedha za Serikali kwa kuwaleta mashahidi hao, kwani nao hawana kitu tofauti na mashahidi wengine,” alidai Mtikila.

Hakimu Mugeta alisema uamuzi wa Mtikila ni mzuri, asipoteze fedha za umma kama anaamini hivyo atasoma hukumu leo.

Mtikila ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, alidai kuwa, kesi hiyo ilifunguliwa kutokana na chuki zilizokuwapo kati yake na mchungaji mwenzake, lakini kwa upande wa Rais Kikwete hakumshitaki pamoja na kwamba alimpa nakala ya waraka huo unaodaiwa wa uchochezi.

Shahidi wa pili wa upande wa utetezi, Mpoki Bukuku kutoka Gazeti la Mwananchi, alidai mahakamani hapo kwamba, walichapisha habari yenye kichwa cha habari ‘Mtikila apiga kampeni kanisani kumpinga Kikwete’.

Pia alidai kwamba, gazeti hilo liliandika Mtikila achunguzwa na Polisi kwa kumwaga sumu, Rais Kikwete asichaguliwe mwaka 2010 na kuongeza kuwa habari hiyo iliripoti kilichotokea Mwanza na ilikuwa ya kweli kwa sababu kati ya polisi na Mtikila, hakuna aliyekanusha.

Alidai habari hiyo, ilikuwa ikielezea mafundisho waliyokuwa wakitoa viongozi wa dini katika kongamano.

Mtikila, anadaiwa Aprili, 2010 mjini Dar es Salaam, alisambaza waraka anaodai wa kuunusuru Ukristo wenye lengo la kuangamizwa na Jihad ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba Wakristo wajitoe muhanga kukomesha ugaidi.

Alidai waraka uliosambazwa, alisaini akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya kuunusuru Ukristo na walichapa nakala 100,000, lakini aligoma kutaja mahali walipochapishia nakala hizo.

Maelezo yote hayo yalitolewa mahakamani kama kielelezo na SSP, Ibeleze Mrema aliyemuhoji Mtikila Aprili 14, 2010 na alipotakiwa kueleza chochote kuhusu kielelezo hicho, mshitakiwa alisema hana swali na akakubali kipokelewe na mahakama.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa