Home » » RISASI, MABOMU VYARINDIMA DAR

RISASI, MABOMU VYARINDIMA DAR



Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

RISASI za moto, mabomu ya machozi, jana vilirindima katika Kijiji cha Nakasangwe, kilichoko Kata ya Tegeta, nje ya kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Hali hiyo ilitokea wakati askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari kanzu na askari wengine walipokuwa wakipambana na wavamizi wa kijiji hicho. Wakati wa operesheni hiyo iliyokwenda sambamba na ubomoaji wa nyumba, askari hao walishirikiana na mgambo wa Manispaa ya Kinondoni ambao walikuwa wakitumia virungu kupambana na wananchi hao.

Wakati wa operesheni hiyo, kulikuwa na magari zaidi ya 60 pamoja na wafanyakazi kutoka idara mbalimbali za serikali jijini Dar es Salaam zaidi ya 1,000, ambao wote walikuwa na jukumu la kuwahamisha kwa nguvu wavamizi hao, maarufu kwa jina la Mungiki.

Operesheni hiyo ilianza jana saa moja asubuhi na kulikuwa na upinzani mkali baina ya polisi na wananchi ambao walikuwa hawataki kuhama katika kijiji hicho.

Kabla ya mapambano hayo, wananchi walipata taarifa za ujio wa askari polisi na polisi hao walipofika njia panda ya kwenda katika kijiji hicho jirani na Shule ya Msingi Nakasangwe, walikuta magogo, mawe na mbao zilizokuwa zimepangwa barabarani, huku zikiwa zimepigiliwa misumari.

Wananchi hao waliwatega polisi ili watakapojaribu kupita na magari yao, matairi yatobolewe na misumari hiyo, lakini jaribio hilo halikufanikiwa, baada ya askari polisi kushuka kwenye magari yao na kuanza kuondoa vizuizi vyote vilivyokuwa barabarani.

Baada ya wananchi hao kuona mtego wao umeshindwa kunasa, walibuni mbinu nyingine ambapo walianza kuchoma moto barabarani na kwenye mapori ili kuwazuia polisi wasiendelee na shughuli waliyotarajia kuifanya.

Hata hivyo, njia hiyo nayo haikuzaa matunda, kwani askari hao pamoja na watumishi wa serikali, walifanikiwa kuzima moto huo na kuelekea katika kijiji hicho.

Wananchi hao zaidi ya 1,000 walipoona mbinu zao hazikuzaa matunda, walianza kurusha mawe na mishale mfululizo, lengo kuu likiwa ni kuwazuia polisi na wenzao wasiingie kijijini hapo.

Wakati wa mtafaruku huo, kwa bahati mbaya askari mmoja alichomwa na mshale tumboni, ingawa hakujeruhiwa kutokana na mavazi ya kijeshi aliyokuwa amevaa.

Askari polisi walipoona upinzani unazidi kushika kasi, nao walilazimika kujibu mapigo na kuanza kurusha mabomu ya machozi na risasi hewani ili kuwatawanya watu hao ambao walikuwa tayari kwa mapambano.

Baada ya askari hao kuanza kujibu mapigo, hatimaye wananchi walizidiwa nguvu na kukimbilia katika Kijiji jirani cha Kazaroho na Benako, huku wakiendelea kuwarushia mawe polisi.

Polisi walifanikiwa kuingia katika kijiji hicho na kuanza kubomoa nyumba za wananchi pamoja na mabanda yao ya biashara, hali ambayo ilisababisha baadhi ya wananchi kunufaika na bidhaa zilizokuwamo ndani, ikiwemo vinywaji, mifuko ya saruji na mali nyinginezo.

Kundi hilo hatari ambalo limegawanyika katika makundi 10, limejipatia umaarufu kutokana na vitendo mbalimbali vya kinyama.

Katika kijiji hicho, wavamizi hao wameunda makundi mbalimbali yenye majina ya Kova, Butiama, Tariban, Nyerere, Mungiki, Kijicho, Arufan na mengineyo.

Pamoja na wananchi hao kutimua mbio, polisi waliendelea kurusha mabomu muda wote wa operesheni hiyo ilidumu kwa masaa kadhaa kwa kuwa wavamizi hao walikuwa wakirejea taratibu.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kwamba, wamegundua uhalifu uliokuwa ukiendelea ndani ya kijiji hicho na kukamata watuhumiwa kadhaa.

Alisema operesheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ambapo wamiliki halali wameshinda kesi zaidi ya saba na linasimamiwa na dalali Msolopa Auction Mart aliyepewa kazi na Mahakama.

Kwa mujibu wa Kenyela, awali wamiliki halali waliligawa eneo hilo kwa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) chini ya Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali.

Hata hivyo, NDC lilishindwa kuendeleza miradi hiyo na kuanzia hapo wavamizi wakaingia bila kufuata taratibu.

“Katika operesheni hii tumebaini mambo mengi, ikiwemo asilimia 90 ya wananchi waliokuwa wakiishi hapo kuwa ni raia wa kigeni kutoka nchi za jirani ambapo wamewakabidhi taarifa zao kwa Idara ya Uhamiaji wilaya ili walishughulikie suala hilo.

“Watuhumiwa hao wamekuwa wakijitambulisha kuwa wametoka Bukoba na Kigoma na baadhi yao walikutwa na paspoti za nchi za nje pamoja na fedha za nchi za nje.

“Pamoja na hayo, tunawashikilia watuhumiwa zaidi ya 20 na vielelezo kadhaa na wahusika tutawafikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

“Mwaka jana tulifika katika eneo hilo na viongozi wa ardhi wilaya kwa ajili ya kuwaondoa, lakini zoezi hilo lilishindikana baada ya kuwepo mambo yasiyofaa.

"Kwa kifupi nasema hawa watu ni hatari sana, hawafai, kwani ni wanyama na wamekuwa wakishiriki katika matukio mbalimbali, hata mimi na maofisa ardhi walishawahi kututeka na tusingetumia busara wangetuua siku ile," alisema Kamanda Kenyela.

Alisema nyumba zilizovunjwa ni zaidi ya 200 ambapo wavamizi hao wamevamia zaidi ya ekari 300 hadi 400 na kwa Kata ya Bunju na Tegeta wamevamia zaidi ya ekari 10,000.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alisema operesheni hiyo ni endelevu na imepewa baraka na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa wa Dar es Salaam.

“Vijiji vilivyovamiwa ni Kinondo, Nakasangwe, Madale, Mabwepande na Kazaroho na Serikali itaendelea kuwaondoa kwa amani ili kuepusha damu kumwagika.

“Baada ya mashamba hayo kurejeshwa kwa wamiliki wa awali, Serikali itakaa na wamiliki hao Agosti 24, mwaka huu kujadili suala la mipango miji.

"Haiwezekani mtu akaendelea kumiliki shamba ekari zaidi ya 10 katikati ya mji, hapa kinachotakiwa sasa ni kuwarejeshea mashamba yao halafu tutajadiliana nao namna ya kupanga mipango miji," alisema Rugimbana.

Hata hivyo aliwashauri wananchi kuacha kununua mashamba bila kuwashirikisha viongozi wa serikali ili kuepuka kutapeliwa.

Alisema operesheni hiyo imegharimu zaidi ya Sh milioni 12, hivyo ni muda muafaka kwa jamii kuacha kuvamia maeneo ili kuepusha hasara kwa serikali.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick, alisema ameruhusu operesheni hiyo ifanyike.

Mmoja wa wamiliki wa eneo hilo ambaye pia ni Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Philipsi Bwathondi, alisema katika eneo lililokuwa limevamiwa anamiliki ekari 13 na amepanda mazao mbalimbali ambapo lilivamiwa na wavamizi hao tangu mwaka 2007.

Habari hii imeandaliwa na Christina Gauluhanga, Asifiwe George na Sebastian Mparazo.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa