na Nasra Abdallah
BARAZA la
Waganga Watafiti wa Tiba Asilia nchini (BAWATA), limeitaka serikali sasa
kugeukia dawa asili za kurefusha maisha (ARV’s) kwa watu wanaoishi na virusi
vya ukimwi, ili kuepuka matatizo yanayojitokeza kwa kutumia dawa za kisasa.
Tamko la
waganga hao linakuja ikiwa ni siku chache tangu kutolewa kwa habari inayohusu
kuwapo kwa ARV’s feki nchini na kuwaletea madhara makubwa watumiaji.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bawata, Dk.
Abdallah Mandai, alisema hawaoni sababu za serikali kuendelea kuagiza dawa hizo
kutoka nje ya nchi wakati dawa za asili zipo.
Mandai alisema
dawa za asili hazina muda wa kuisha matumizi kama ilivyo kwa dawa za kisasa na
wala hazileti madhara kwa mtumiaji.
Kwa mujibu wa
mganga huyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu katika kituo chake ameshapokea
wagonjwa wapatao 30 ambao wamedhurika na dawa za kuongeza maisha na kuongeza
kuwa alipowapatia dawa yake ya kuondoa sumu, wamepona na kurudi katika hali zao
za kawaida.
“Kwa kweli mimi
bado sioni sababu ya serikali kung’ang’ania kuagiza dawa hizo nje ya nchi,
badala yake kinachotakiwa ni kushirikiana nasi kwa karibu ili kuona tunatatua
tatizo hili na sio kutudharau kama wanavyofanya sasa,” alisema.
Pia Mandai
alitumia fursa hiyo kutangaza nia yake ya kuwatibu bure wale wote ambao wanajua
wamepata madhara ya dawa hizo kama njia mojawapo ya kuwasaidia.
Chanzo: Tanania Daima
No comments:
Post a Comment