na Shehe Semtawa
BAADHI ya
wateja na wafanyakazi wa ofisi za Halmashauri ya Jiji Wilaya ya Ilala, Dar es
Salaam, afya zao ziko hatarini kupata maradhi ya mlipuko kutokana na choo cha
hoteli iliyomo katika jengo hilo kufurika hadi kutiririsha kinyesi nje.
Wakizungumza na
Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, walisema wanastaajabishwa na hali
hiyo ya hatari ikiendelea kwa zaidi ya miezi mitano bila kutafutiwa ufumbuzi.
Mmoja wa wateja
hao, Khamisi Khalfan alisema kutokana na uchafu huo kukithiri na kuhatarisha
afya zao baadhi yao wanatarajia kuacha kwenda kujipatia huduma katika hoteli
hiyo.
Mfanyakazi
mmoja wa ofisi hiyo aliyekataa kutajwa, alisema tatizo hilo linafahamika muda
mrefu, lakini inatia hofu kuwaona viongozi wakikaa kimya kama vile hawana
taarifa za uchafu.
“Unajua hiki
choo tangu kuanza kufurika ilikuwa mwenzi wa nne ambapo hata mkurugezi mwenyewe
wa jiji alifika kujionea hali hiyo, lakini hajachukua hatua,” alisema.
Alisema Agosti,
mwaka huu, mkurugenzi aliwaahidi waendeshaji wa hoteli hiyo kuwa ofisi yake
ingelifanyia kazi haraka tatizo hilo, lakini hadi leo bado halijapatiwa suluhu.
Alipoulizwa
msemaji wa jiji, Gaston Makwembe, kuhusu suala hilo, alisema yuko kwenye ziara
ila waulizwe wenye hoteli hiyo, mkataba wao unasemaje.
Mmoja wa
viongozi katika hoteli hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini,
alikiri kufurika kwa choo hicho, lakini hakuwa akijua mkataba unasemaje iwapo
choo kingefurika nani angehusika kukifanyia usafi, zaidi alisema asubiriwe
mkurugenzi wa hoteli hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment