na Betty Kangonga
WIZARA ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
imetangaza kufanya msako kwa watu wanaochapisha ramani za Tanzania kinyume na
taratibu ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkurugenzi wa
Upimaji na Ramani wa wizara hiyo, Dk. Selassie Mayunga, alibainisha hayo jijini
Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka kisheria ya
kuchapisha ramani hizo na kuzisambaza.
“Tunatangaza
rasmi ramani hizo ni feki hazitakiwi kutumiwa na watakaobainika kuzisambaza
sheria itafuata mkondo wake,” alisema Mayunga.
Alisema
watashirikiana na Jeshi la Polisi kuwakamata wahusika na kuziondoa ramani hizo
kwenye mzunguko.
Aidha,
alileleza kuwa jambo la kusikitisha ni kuwa hata taasisi za umma na binafsi
zinatumia ramani hizo bila kufahamu kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
“Ramani halali
ni ile iliyotolewa na kuchapishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi tu na si vinginevyo,” alisema.
Katika hatua
nyinginge, wizara hiyo imetoa ramani mpya itakayojumuisha mikoa na wilaya
zilizotangazwa na serikali hivi karibuni.
Mwaka jana
serikali ilitangaza mikoa mipya minne ambayo ni Njombe, Geita, Simiyu, Katavi
na wilaya 19.
Mkurugenzi huyo
alisema taasisi za serikali na watu binafsi wanatakiwa kuwasiliana na wizara
hiyo kwa ajili ya kupata ramani hizo halali.
Wakati huohuo,
wizara hiyo imesema migogoro mingi ya ardhi inasababishwa kwa kiasi kikubwa na
baadhi ya wapima ardhi wanaofanya kazi zao bila kufuata taratibu na sheria.
Mkurugenzi huyo
alisema watumishi watakaobainika kufanya makosa hao watafukuzwa kazi mara moja.
“Fanyeni kazi
kwa kufuata misingi ya sheria, atakayekiuka hatakuwa miongoni mwetu,” alisema
Dk. Mayunga.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment