Home » » TBL YAWATAHADHARISHA WANYWAJI WA BIA

TBL YAWATAHADHARISHA WANYWAJI WA BIA

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), imepongezwa kwa kuwasisitiza wateja wake wakiwamo madereva, kuchukua tahadhari wanapokuwa wanaendesha magari huku wakiwa wamelewa.

Pamoja na pongezi hizo, Jeshi la Polisi limesema halitasita kuwachukulia hatua madereva wanaosababisha ajali kutokana na ulevi.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, Johansen Kahatano, aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelea kiwanda hicho cha bia jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani.

Kahatano alisema kwamba, rekodi za polisi zinaonyesha kuna idadi ndogo ya ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva walevi.

Aliongeza kwamba, licha ya uchache wa ajali hizo, kuna kila sababu ya kuamini idadi hiyo inaweza kuongezeka, hivyo kuna haja ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Alisema kwamba, kuna baadhi ya ajali ambazo hutokea na haziandikwi pia zipo zinazoandikwa, lakini chanzo halisi cha ajali hakitambuliwi.

"Tunapokea kesi za ajali kila siku, zipo ajali zinazosababishwa na ulevi na mara nyingine hupuuzwa kwa kutozifikisha kwenye mamlaka husika," alisema Kahatano.

Kuhusu TBL, alisema sera za kampuni hiyo ni nzuri, kwa kuwa kampuni hiyo imeweza kuchukua jukumu la kuhakikisha wateja wao wakiwamo madereva, wanakunywa bia lakini pia watambue wajibu wao.

Naye Mkurugenzi wa Sheria wa TBL, Stephen Kilindo, alisema ni utaratibu wa TBL kuwasilisha taarifa ambayo itawezesha watumiaji wake kuchukua uamuzi mzuri.

"Kama mabalozi, ni wajibu wetu sote kuwafahamisha na kutoa ujumbe na sera za kampuni kwa sababu watumiaji wa bidhaa zetu ni familia zetu na marafiki zetu,” alisema.

Alisema kwamba, TBL inaendelea kufanya kazi kwa karibu na Jeshi la Polisi, ili kuhakikisha watu wanakunywa pombe kwa kuwajibika na kwamba hawanywi na kuendesha magari.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa